Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 9

9
1Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji
na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi!
Ningelia usiku na mchana
kwa kuuawa kwa watu wangu.
2Laiti ningekuwa na nyumba
ya kukaa wasafiri jangwani,
ningewaacha watu wangu
na kwenda mbali nao,
kwa kuwa wote ni wazinzi,
kundi la watu wadanganyifu.
3“Huweka tayari ndimi zao kama upinde,
ili kurusha uongo;
wamekuwa na nguvu katika nchi
lakini si katika ukweli.
Wanatoka dhambi moja hadi nyingine,
hawanitambui mimi,”
asema Mwenyezi Mungu.
4“Jihadhari na rafiki zako;
usiwaamini ndugu zako.
Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu,
na kila rafiki ni msingiziaji.
5Rafiki humdanganya rafiki,
hakuna yeyote asemaye kweli.
Wamefundisha ndimi zao kudanganya,
wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi.
6Unakaa katikati ya udanganyifu;
katika udanganyifu wao wanakataa kunitambua mimi,”
asema Mwenyezi Mungu.
7Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:
“Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu,
kwani ni nini kingine niwezacho kufanya
kwa sababu ya dhambi ya watu wangu?
8Ndimi zao ni mshale wenye sumu,
hunena kwa udanganyifu.
Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake,
lakini moyoni mwake humtegea mtego.
9Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?”
asema Mwenyezi Mungu.
“Je, nisijilipizie kisasi
kwa taifa kama hili?”
10Nitalia na kuomboleza kwa ajili ya milima
na kuomboleza kuhusu malisho ya jangwani.
Yamekuwa ukiwa, wala hakuna apitaye humo,
milio ya ng’ombe haisikiki.
Ndege wa angani wametoroka
na wanyama wamekimbia.
11“Nitaifanya Yerusalemu lundo la magofu,
makao ya mbweha;
nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa,
asiwepo atakayeishi humo.”
12Ni mtu yupi aliye na hekima ya kutosha ayaelewe haya? Ni nani aliyefundishwa na Mwenyezi Mungu awezaye kuyaeleza haya? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa ukiwa kama jangwa ambapo hakuna awezaye kupita?
13Mwenyezi Mungu akasema, “Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu, niliyoiweka mbele yao: hawajaniheshimu mimi wala kufuata sheria yangu. 14Badala yake wamefuata ukaidi wa mioyo yao, wamefuata Mabaali, kama baba zao walivyowafundisha.” 15Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: “Tazama, nitawafanya watu hawa wale chakula kichungu na kunywa maji yenye sumu. 16Nitawatawanya katika mataifa ambayo wao wala baba zao hawakuyajua, nikiwafuata kwa upanga hadi niwaangamize kabisa.”
17Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:
“Fikiri sasa! Waite wanawake waombolezaji waje,
waite wale walio na ustadi kati yao.
18Nao waje upesi
waomboleze juu yetu,
hadi macho yetu yatiririke machozi
na kope zetu zibubujike maji.
19Sauti ya kuomboleza imesikika kutoka Sayuni:
‘Tazama jinsi tulivyoangamizwa!
Tazama jinsi aibu yetu ilivyo kubwa!
Ni lazima tuihame nchi yetu
kwa sababu nyumba zetu zimekuwa magofu.’ ”
20Basi, enyi wanawake, sikieni neno la Mwenyezi Mungu;
fungueni masikio yenu msikie maneno ya kinywa chake.
Wafundisheni binti zenu kuomboleza;
fundishaneni kila mmoja na mwenzake maombolezo.
21Mauti imeingia ndani kupitia madirishani,
imeingia kwenye majumba yetu ya fahari;
imewakatilia mbali watoto katika barabara
na vijana wa kiume kutoka viwanja vya miji.
22Sema, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“ ‘Mizoga ya watu italala
kama kinyesi katika mashamba,
kama malundo ya nafaka nyuma ya mvunaji,
wala hakuna atakayeikusanya.’ ”
23Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,
au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,
wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,
24lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hii:
kwamba ananifahamu na kunijua mimi,
kwamba mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitendaye wema,
hukumu na haki duniani,
kwa kuwa napendezwa na haya,”
asema Mwenyezi Mungu.
25“Siku zinakuja, nitakapowaadhibu wale wote ambao wametahiriwa kimwili tu, asema Mwenyezi Mungu, 26yaani Misri, Yuda, Edomu, Amoni, Moabu na wote wanaoishi jangwani sehemu za mbali. Kwa maana mataifa haya yote hayakutahiriwa mioyo yao, nayo nyumba yote ya Israeli haikutahiriwa.”

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 9: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia