Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 10

10
Mwenyezi Mungu na sanamu
1Sikieni lile Mwenyezi Mungu anasema nanyi, ee nyumba ya Israeli. 2Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Usijifunze njia za mataifa
wala usitishwe na ishara katika anga,
ingawa mataifa yanatishwa nazo.
3Kwa maana desturi za mataifa hazina maana,
wanakata mti msituni,
na fundi anauchonga kwa patasi.
4Wanauremba kwa fedha na dhahabu,
wanaukaza kwa nyundo na misumari ili usitikisike.
5Sanamu zao ni kama kinyago
kilichowekwa katika shamba la matango kutishia ndege,
nazo haziwezi kuongea;
na kwa kuwa haziwezi kutembea zinabebwa.
Usiziogope. Haziwezi kudhuru
wala kutenda lolote jema.”
6Hakuna aliye kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu;
wewe ni mkuu,
jina lako ni lenye nguvu na uweza.
7Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe,
Ee Mfalme wa mataifa?
Hii ni stahili yako.
Miongoni mwa watu wote wenye hekima
katika mataifa na katika falme zao zote,
hakuna aliye kama wewe.
8Wote hawana akili, tena ni wapumbavu;
wanafundishwa na sanamu batili za miti.
9Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi
na dhahabu kutoka Ufazi.
Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza
huvikwa mavazi ya rangi ya samawi na urujuani:
vyote vikiwa vimetengenezwa
na mafundi stadi.
10Lakini Mwenyezi Mungu ni Mungu wa kweli,
yeye ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele.
Anapokasirika, dunia hutetemeka,
mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.
11“Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia duniani na chini ya mbingu.’ ”
12Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake,
akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake,
na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.
13Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;
huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia.
Hupeleka miali ya radi pamoja na mvua,
naye huuleta upepo kutoka ghala zake.
14Kila mtu ni mjinga na hana maarifa;
kila sonara ameaibishwa na sanamu zake.
Vinyago vyake ni vya udanganyifu;
havina pumzi.
15Ni ubatili tu, vitu vya kufanyia mzaha;
wakati wa hukumu yao, wataangamia.
16Yeye aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo,
kwani ndiye Muumba wa vitu vyote,
pamoja na Israeli, kabila la urithi wake:
Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake.
Maangamizi yajayo
17Kusanyeni mali na vitu vyenu mwondoke nchi hii,
enyi mnaoishi katika hali ya kuzingirwa na jeshi.
18Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Wakati huu, nitawatupa nje kwa nguvu
wote wanaoishi katika nchi hii;
nitawataabisha
ili wapate kutekwa.”
19Ole wangu mimi kwa ajili ya kuumia kwangu!
Jeraha langu ni kubwa!
Lakini nilisema,
“Kweli hii ni adhabu yangu,
nami sharti niistahimili.”
20Hema langu limeangamizwa;
kamba zake zote zimekatwa.
Wana wangu wametekwa na hawapo tena;
hakuna hata mmoja aliyebaki wa kusimamisha hema langu
wala wa kusimamisha kibanda changu.
21Wachungaji hawana akili
wala hawamuulizi Mwenyezi Mungu,
hivyo hawastawi
na kundi lao lote la kondoo limetawanyika.
22Sikilizeni! Taarifa inakuja:
ghasia kubwa kutoka nchi ya kaskazini!
Hii itafanya miji ya Yuda ukiwa,
na kuwa makao ya mbweha.
Maombi ya Yeremia
23Ninajua, Ee Mwenyezi Mungu, kwamba maisha ya mwanadamu si yake mwenyewe;
hawezi kuziongoza hatua zake mwenyewe.
24Unirudi, Ee Mwenyezi Mungu, lakini kwa kipimo cha haki:
si katika hasira yako,
usije ukaniangamiza.
25Umwage ghadhabu yako juu ya mataifa
wasiokujua wewe,
juu ya mataifa wasioliitia jina lako.
Kwa kuwa wamemwangamiza Yakobo;
wamemwangamiza kabisa
na kuiharibu nchi yake.

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 10: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia