Yeremia 42:1-12
Yeremia 42:1-12 NEN
Ndipo maafisa wote wa jeshi, pamoja na Yohanani mwana wa Karea, na Yezania mwana wa Hoshaya, na watu wote kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana wakamjia Yeremia nabii na kumwambia, “Tafadhali sikia maombi yetu na umwombe BWANA Mungu wako kwa ajili ya watu hawa wote waliosalia. Kwa kuwa kama unavyoona sasa, ingawa wakati fulani tulikuwa wengi, sasa tumesalia wachache tu. Omba ili BWANA Mungu wako atuambie twende wapi na tufanye nini.” Nabii Yeremia akajibu, “Nimewasikia. Kwa hakika nitamwomba BWANA Mungu wenu kama mlivyoomba. Nitawaambia kila kitu asemacho BWANA, wala sitawaficha chochote.” Kisha wakamwambia Yeremia, “BWANA na awe shahidi wa kweli na mwaminifu kati yetu kama hatutafanya sawasawa na kila kitu BWANA Mungu wako atakachokutuma utuambie. Likiwa jema au likiwa baya, tutamtii BWANA Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake, ili mambo yote yawe mema kwetu, kwa maana tutamtii BWANA Mungu wetu.” Baada ya siku kumi, neno la BWANA likamjia Yeremia. Kwa hiyo akawaita pamoja Yohanani mwana wa Karea, na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye na watu wote kuanzia mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana. Akawaambia, “Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kuwasilisha maombi yenu: ‘Kama mkikaa katika nchi hii, nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawangʼoa, kwani ninahuzunishwa na maafa niliyowapiga nayo. Msimwogope mfalme wa Babeli, ambaye sasa mnamwogopa. Msimwogope, asema BWANA, kwa kuwa niko pamoja nanyi, nami nitawaokoa na kuwaponya kutoka mikononi mwake. Nitawaonea huruma ili naye awe na huruma nanyi na kuwarudisha katika nchi yenu.’