Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 42:1-12

Yeremia 42:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo makamanda, wote wa majeshi, na Yohana, mwana wa Karea, na Yezania, mwana wa Hoshaya, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa, wakakaribia, wakamwambia Yeremia, nabii, Twakusihi, maombi yetu yakubaliwe mbele yako, ukatuombee kwa BWANA, Mungu wako, yaani, watu hawa wote waliosalia; maana tumesalia wachache tu katika watu wengi, kama macho yako yatuonavyo; ili kwamba BWANA, Mungu wako, atuoneshe njia ambayo yatupasa tuiendee, na jambo litupasalo tulitende. Ndipo Yeremia, nabii, akawaambia, Nimewasikia; tazama, nitamwomba BWANA, Mungu wenu, sawasawa na maneno yenu; tena itakuwa, neno lolote ambalo BWANA atawajibu, nitawaambia; sitawazuilia neno liwalo lote. Wakamwambia Yeremia, BWANA na awe shahidi wa kweli na uaminifu kati yetu; ikiwa hatufanyi sawasawa na neno lile, ambalo BWANA, Mungu wako, atakutuma utuletee. Likiwa jema, au likiwa baya, sisi tutaitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake; ipate kuwa faida yetu, tunapoitii sauti ya BWANA, Mungu wetu. Ikawa, baada ya siku kumi, neno la BWANA likamjia Yeremia. Ndipo akamwita Yohana, mwana wa Karea, na makamanda wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa, akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kwake, ili niyaweke maombi yenu mbele yake, asema hivi; Ikiwa mtabaki katika nchi hii, ndipo nitawajenga, wala sitawabomoa, nami nitawapanda, wala sitawang'oa; kwa maana nayajutia mabaya niliyowatenda. Msimwogope mfalme wa Babeli, mnayemwogopa; msimwogope, asema BWANA; maana mimi ni pamoja nanyi, niwaokoe, na kuwaponya kutoka kwa mkono wake. Nami nitawapa rehema, kwamba awarehemu ninyi, na kuwarudisha mkae katika nchi yenu wenyewe.

Shirikisha
Soma Yeremia 42

Yeremia 42:1-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ndipo maafisa wote wa jeshi, pamoja na Yohanani mwana wa Karea, na Yezania mwana wa Hoshaya, na watu wote kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana wakamjia Yeremia nabii na kumwambia, “Tafadhali sikia maombi yetu na umwombe BWANA Mungu wako kwa ajili ya watu hawa wote waliosalia. Kwa kuwa kama unavyoona sasa, ingawa wakati fulani tulikuwa wengi, sasa tumesalia wachache tu. Omba ili BWANA Mungu wako atuambie twende wapi na tufanye nini.” Nabii Yeremia akajibu, “Nimewasikia. Kwa hakika nitamwomba BWANA Mungu wenu kama mlivyoomba. Nitawaambia kila kitu asemacho BWANA, wala sitawaficha chochote.” Kisha wakamwambia Yeremia, “BWANA na awe shahidi wa kweli na mwaminifu kati yetu kama hatutafanya sawasawa na kila kitu BWANA Mungu wako atakachokutuma utuambie. Likiwa jema au likiwa baya, tutamtii BWANA Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake, ili mambo yote yawe mema kwetu, kwa maana tutamtii BWANA Mungu wetu.” Baada ya siku kumi, neno la BWANA likamjia Yeremia. Kwa hiyo akawaita pamoja Yohanani mwana wa Karea, na maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye na watu wote kuanzia mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana. Akawaambia, “Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kuwasilisha maombi yenu: ‘Kama mkikaa katika nchi hii, nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawangʼoa, kwani ninahuzunishwa na maafa niliyowapiga nayo. Msimwogope mfalme wa Babeli, ambaye sasa mnamwogopa. Msimwogope, asema BWANA, kwa kuwa niko pamoja nanyi, nami nitawaokoa na kuwaponya kutoka mikononi mwake. Nitawaonea huruma ili naye awe na huruma nanyi na kuwarudisha katika nchi yenu.’

Shirikisha
Soma Yeremia 42

Yeremia 42:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha makamanda wote wa majeshi, Yohanani mwana wa Karea, na Azaria mwana wa Heshaia pamoja na watu wote, wadogo kwa wakubwa, wakamwendea Yeremia, wakamwambia, “Tafadhali sikiliza maombi yetu na kutuombea dua kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, sisi sote tuliosalia (kwa maana tulikuwa wengi, lakini sasa tumebaki wachache tu, kama uonavyo). Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na atuoneshe njia anayotaka tuifuate, na kile anachotaka tukifanye.” Yeremia akawajibu, “Vema; nimesikia. Nitamwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kama mlivyonisihi; jibu lolote atakalonipa Mwenyezi-Mungu, nitawaambieni; sitawaficha chochote.” Kisha, watu wakamwambia Yeremia, “Mwenyezi-Mungu na awe shahidi wa kweli na mwaminifu dhidi yetu ikiwa hatutafanya jinsi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atakavyokuagiza utuambie. Iwe ni jambo la kupendeza au la, sisi tutaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu ambaye tunakutuma kwake ili tufanikiwe tutakapomtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.” Baada ya siku kumi, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia. Basi, Yeremia akamwita Yohanani mwana wa Karea, na makamanda wote wa majeshi pamoja na watu wote, wadogo kwa wakubwa, akawaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli ambaye mlinituma kwake nipeleke maombi yenu, asema hivi: Kama mtabaki katika nchi hii, basi, nitawajenga, wala sitawabomoa; nitawaotesha wala sitawangoa; kwa maana nitabadili nia kwa sababu ya maafa niliyowatenda. Msimwogope mfalme wa Babuloni mnayemwogopa; naam, msimwogope hata kidogo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mimi niko pamoja nanyi kuwaokoeni na kuwasalimisha kutoka mikononi mwake. Nitawahurumieni na kumfanya mfalme awahurumie na kuwaacha nchini mwenu.

Shirikisha
Soma Yeremia 42

Yeremia 42:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo maakida wote wa majeshi, na Yohana, mwana wa Karea, na Yezania, mwana wa Hoshaya, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa, wakakaribia, wakamwambia Yeremia, nabii, Twakusihi, maombi yetu yakubaliwe mbele yako, ukatuombee kwa BWANA, Mungu wako, yaani, watu hawa wote waliosalia; maana tumesalia wachache tu katika watu wengi, kama macho yako yatuonavyo; ili kwamba BWANA, Mungu wako, atuonyeshe njia ambayo yatupasa tuiendee, na jambo litupasalo tulitende. Ndipo Yeremia, nabii, akawaambia, Nimewasikia; tazama, nitamwomba BWANA, Mungu wenu, sawasawa na maneno yenu; tena itakuwa, neno lo lote ambalo BWANA atawajibu, nitawaambia; sitawazuilia neno liwalo lote. Wakamwambia Yeremia, BWANA na awe shahidi wa kweli na uaminifu kati yetu; ikiwa hatufanyi sawasawa na neno lile, ambalo BWANA, Mungu wako, atakutuma utuletee. Likiwa jema, au likiwa baya, sisi tutaitii sauti ya BWANA, Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake; ipate kuwa faida yetu, tunapoitii sauti ya BWANA, Mungu wetu. Ikawa, baada ya siku kumi, neno la BWANA likamjia Yeremia. Ndipo akamwita Yohana, mwana wa Karea, na maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa, akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kwake, ili niyaweke maombi yenu mbele yake, asema hivi; Ikiwa mtakaa bado katika nchi hii, ndipo nitawajenga, wala sitawabomoa, nami nitawapanda, wala sitawang’oa; kwa maana nayajutia mabaya niliyowatenda. Msimwogope mfalme wa Babeli, mnayemwogopa; msimwogope, asema BWANA; maana mimi ni pamoja nanyi, niwaokoe, na kuwaponya na mkono wake. Nami nitawapa rehema, kwamba awarehemu ninyi, na kuwarudisha mkae katika nchi yenu wenyewe.

Shirikisha
Soma Yeremia 42