Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 35

35
Warekabi wasifiwa
1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wakati wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda: 2“Nenda kwa jamaa ya Warekabi, uwaalike waje kwenye moja ya vyumba vya pembeni vya nyumba ya Mwenyezi Mungu, na uwape divai wanywe.”
3Basi nikaenda kumwita Yaazania mwana wa Yeremia, mwana wa Habazinia, na ndugu zake na wanawe wote, yaani jamaa nzima ya Warekabi. 4Nikawaleta katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, ndani ya chumba cha wana wa Hanani mwana wa Igdalia mtu wa Mungu. Kilikuwa karibu na chumba cha maafisa, kilichokuwa juu ya kile cha Maaseya mwana wa Shalumu, aliyekuwa bawabu. 5Kisha nikaweka mabakuli yaliyojaa divai na baadhi ya vikombe mbele ya watu wa jamaa ya Warekabi na kuwaambia, “Kunyweni divai.”
6Lakini wao wakajibu, “Sisi hatunywi divai, kwa sababu baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu, alitupatia agizo hili: ‘Ninyi wala wazao wenu msinywe divai. 7Pia msijenge nyumba wala kuotesha mbegu au kupanda mashamba ya mizabibu. Kamwe msiwe na kitu chochote katika hivi, bali mtaishi katika mahema. Ndipo mtakapoishi kwa muda mrefu katika nchi ambayo ninyi ni wahamiaji.’ 8Tumetii kila kitu ambacho baba yetu Yonadabu mwana wa Rekabu alituamuru. Sisi wenyewe, wake zetu, watoto wetu wa kiume na wa kike hatujawahi kunywa divai, 9wala kujenga nyumba za kuishi au kuwa na mashamba ya mizabibu, mashamba au mazao. 10Tumeishi katika mahema na tumetii kikamilifu kila kitu alichotuamuru baba yetu Yonadabu. 11Lakini wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli alipoivamia nchi hii, tulisema, ‘Njooni, lazima twende Yerusalemu ili kukimbia majeshi ya Wakaldayo na ya Washamu.’ Kwa hiyo tumeishi Yerusalemu.”
12Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema: 13“Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, aliye Mungu wa Israeli, asemalo: Nenda ukawaambie watu wa Yuda na watu wa Yerusalemu, ‘Je, hamwezi kujifunza kutoka kwa wana wa Rekabu, na kuyatii maneno yangu?’ asema Mwenyezi Mungu. 14‘Yonadabu mwana wa Rekabu aliwaagiza wanawe wasinywe divai, na agizo hilo wamelishika. Hadi leo hawanywi divai, kwa sababu wanatii amri ya baba yao. Nimenena nanyi tena na tena, lakini hamkunitii. 15Mara kwa mara nimewatuma kwenu watumishi wangu wote, manabii wakisema, “Geukeni, kila mmoja aiache njia yake mbaya, na kutengeneza matendo yake. Msiifuate wala kuitumikia miungu mingine. Ndipo mtakapoishi katika nchi niliyowapa ninyi na baba zenu.” Lakini hamkujali wala kunisikiliza. 16Wazao wa Yonadabu mwana wa Rekabu walitimiza amri ambayo baba yao aliwapa, lakini watu hawa hawakunitii mimi.’
17“Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya Yuda na juu ya kila mmoja aishiye Yerusalemu kila aina ya maafa niliyotamka dhidi yao. Nilinena nao, lakini hawakusikiliza. Niliwaita, lakini hawakujibu.’ ”
18Kisha Yeremia akaiambia jamaa ya Warekabi, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: ‘Mmetii amri ya baba yenu Yonadabu, na mmefuata mafundisho yake yote na mmefanya kila kitu alichowaamuru.’ 19Kwa hiyo hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Yonadabu mwana wa Rekabu hatakosa kamwe kuwa na mtu wa kunitumikia mimi.’ ”

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 35: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia