Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 34

34
Onyo kwa Sedekia
1Wakati Nebukadneza mfalme wa Babeli na jeshi lake lote, pamoja na falme zote na mataifa katika himaya aliyotawala walikuwa wakipigana dhidi ya Yerusalemu pamoja na miji yote iliyoizunguka, neno hili lilimjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu: 2“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Nenda kwa Sedekia mfalme wa Yuda umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto. 3Hutaweza kuepuka mkono wake, bali hakika utatekwa na kukabidhiwa kwake. Utamwona mfalme wa Babeli kwa macho yako mwenyewe, naye atazungumza nawe ana kwa ana. Nawe utaenda Babeli.
4“ ‘Lakini sikia ahadi ya Mwenyezi Mungu, ee Sedekia mfalme wa Yuda. Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu wewe: Hutakufa kwa upanga, 5bali utakufa kwa amani. Kama vile watu walivyowasha moto wa maziko kwa heshima ya baba zako, wafalme waliokutangulia, ndivyo watu watakavyowasha moto kwa heshima yako na kuomboleza, wakisema: “Ole, Ee Mwenyezi Mungu!” Mimi mwenyewe ninaweka ahadi hii, asema Mwenyezi Mungu.’ ”
6Ndipo nabii Yeremia akamwambia Sedekia mfalme wa Yuda mambo haya yote huko Yerusalemu, 7wakati jeshi la mfalme wa Babeli lilipokuwa likipigana dhidi ya Yerusalemu na miji mingine ya Yuda iliyokuwa bado imara, yaani Lakishi na Azeka. Hii ilikuwa miji pekee yenye ngome iliyobaki katika Yuda.
Uhuru kwa watumwa
8Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, baada ya Mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote huko Yerusalemu ili kutangaza uhuru kwa watumwa. 9Kila mmoja alipaswa kuwaacha huru watumwa wake Waebrania, wanawake na wanaume. Hakuna yeyote aliyeruhusiwa kumfanya Myahudi mwenzake kuwa mtumwa. 10Kwa hiyo maafisa wote na watu walioingia katika agano hili wakakubali kwamba watawaacha huru watumwa wao wa kiume na wa kike, na hawatawashikilia tena. Wakakubali na wakawaacha huru. 11Lakini baadaye wakabadili mawazo yao, na kuwarudisha wale watumwa waliokuwa wamewaacha huru, wakawafanya tena watumwa.
12Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema: 13“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Nilifanya agano na baba zenu nilipowatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. Nilisema, 14‘Kila mwaka wa saba, kila mmoja wenu ni lazima amwache huru mtumwa ambaye ni Mwebrania mwenzenu aliyejiuza kwenu. Baada ya kukutumikia kwa miaka sita, ni lazima umwache huru aende zake.’#34:14 Kumbukumbu 15:12 Hata hivyo baba zenu hawakunisikiliza wala kunijali. 15Hivi karibuni tu mlitubu na kufanya yaliyo sawa machoni pangu: Kila mmoja wenu aliwatangazia uhuru Waebrania wake. Hata mlifanya agano mbele zangu ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu. 16Lakini sasa mmegeuka na kulinajisi jina langu. Kila mmoja wenu amemrudisha mtumwa wa kiume na wa kike ambao mlikuwa mmewaacha huru waende zao walikotaka. Mmewalazimisha kuwa watumwa wenu tena.
17“Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Hamkunitii mimi. Hamkutangaza uhuru kwa ndugu zenu. Hivyo sasa, ninawatangazia ninyi ‘uhuru,’ asema Mwenyezi Mungu: ‘uhuru’ ili kuanguka kwa upanga, tauni na njaa. Nitawafanya mwe chukizo kwa falme zote za dunia. 18Watu waliovunja agano langu, na ambao hawakutunza masharti ya agano walilofanya mbele zangu, nitawafanya kama ndama waliyemkata vipande viwili, kisha wakatembea kati ya vile vipande vya huyo ndama. 19Viongozi wa Yuda na Yerusalemu, maafisa wa mahakama, makuhani na watu wote wa nchi waliopita kati ya vile vipande vya ndama, 20nitawatia mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao. Maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi.
21“Nitamtia Sedekia mfalme wa Yuda na maafisa wake mikononi mwa adui zao wanaotafuta uhai wao, kwa jeshi la mfalme wa Babeli, lililokuwa limeondoka kwenu. 22Nitatoa amri, asema Mwenyezi Mungu, nami nitawarudisha tena katika mji huu. Watapigana dhidi yake, wautwae na kuuteketeza kwa moto. Nami nitaiangamiza miji ya Yuda ili pasiwe na yeyote atakayeweza kuishi humo.”

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 34: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia