Yeremia 33
33
Ahadi ya kurejeshwa
1Yeremia alipokuwa angali amefungwa kwenye ua wa walinzi, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia mara ya pili kusema: 2“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, yeye aliyeumba dunia, Mwenyezi Mungu aliyeifanya na kuithibitisha, Mwenyezi Mungu ndilo jina lake: 3‘Niite, nami nitakuitikia, nitakuonesha mambo makubwa, yasiyochunguzika na usiyoyajua.’ 4Kwa maana hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu nyumba zilizo mji huu na majumba ya kifalme ya Yuda, zote ambazo zimebomolewa ili zitumiwe kupinga kuzingirwa na jeshi na dhidi ya upanga 5katika kupigana na Wakaldayo: ‘Zitajazwa na maiti za watu nitakaowangamiza kwa hasira na ghadhabu yangu. Nitauficha uso wangu kwa sababu ya maovu yake yote.
6“ ‘Hata hivyo, nitauletea afya na uponyaji, nitawaponya watu wangu na kuwafanya wafurahie amani tele na salama. 7Nitawarudisha Yuda na Israeli kutoka uhamishoni, na kuwajenga tena kama walivyokuwa hapo awali. 8Nitawatakasa dhambi zote walizofanya dhidi yangu, na nitawasamehe dhambi zote za uasi dhidi yangu. 9Kisha mji huu utaniletea utukufu, furaha, sifa na heshima mbele ya mataifa yote ya dunia yatakayosikia mambo yote mazuri ninayoufanyia. Nao watashangaa na kutetemeka kwa ajili ya wingi wa mafanikio na amani nitakayoupatia.’
10“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Mnasema kuhusu mahali hapa kwamba, “Ni mahali palipoachwa ukiwa, pasipo na wanadamu wala wanyama.” Lakini katika miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu ambazo zimeachwa, ambazo hazikaliwi na wanadamu wala wanyama, huko kutasikika kwa mara nyingine 11sauti za shangwe na furaha, sauti za bibi arusi na bwana arusi, na sauti za wale waletao sadaka za shukrani katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, wakisema,
“ ‘ “Mshukuruni Mwenyezi Mungu,
Mungu wa majeshi ya mbinguni,
kwa maana Mwenyezi Mungu ni mwema;
fadhili zake zadumu milele.”
Kwa kuwa nitairudishia nchi baraka kama ilivyokuwa hapo awali,’ asema Mwenyezi Mungu.
12“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Mahali hapa, palipo ukiwa, bila wanadamu wala wanyama: katika miji yake, yatakuwa tena malisho ya wachungaji kuyalaza makundi yao. 13Katika miji ya nchi ya vilima, ya vilima vya magharibi na ya Negebu, katika nchi ya Benyamini, katika vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu na katika miji ya Yuda, makundi ya kondoo yatapita tena chini ya mkono wa yeye anayehesabu,’ asema Mwenyezi Mungu.
14“ ‘Siku zinakuja,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘wakati nitakapotimiza ahadi yangu ya rehema niliyoifanya kwa nyumba ya Israeli na kwa nyumba ya Yuda.
15“ ‘Katika siku hizo na wakati huo
nitalifanya Tawi la haki lichipuke kutoka ukoo wa Daudi,
naye atafanya lile lililo haki na sawa
katika nchi.
16Katika siku hizo, Yuda ataokolewa
na Yerusalemu ataishi salama.
Hili ndilo jina atakaloitwa:
Mwenyezi Mungu ni Haki Yetu.’
17Kwa maana hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Daudi kamwe hatakosa mtu wa kukalia kiti cha utawala cha nyumba ya Israeli, 18wala makuhani, ambao ni Walawi, kamwe hawatakosa mtu wa kusimama mbele zangu daima ili kutoa sadaka za kuteketezwa, sadaka ya nafaka, na dhabihu.’ ”
19Neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema: 20“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Ikiwa mtaweza kuvunja agano langu kuhusu usiku na mchana, ili usiku na mchana visiwepo kwa nyakati zake, 21basi agano langu na Daudi mtumishi wangu, na agano langu na Walawi ambao ni makuhani wanaohudumu mbele zangu, linaweza kuvunjwa, na Daudi hatakuwa tena na mzao wa kutawala kwenye kiti chake cha utawala. 22Nitawafanya wazao wa Daudi mtumishi wangu na Walawi wanaohudumu mbele zangu wengi, wasioweza kuhesabika kama nyota za angani, tena wasiopimika kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.’ ”
23Neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema: 24“Je, hujasikia kwamba watu hawa wanasema, ‘Mwenyezi Mungu amezikataa zile falme mbili alizozichagua’? Kwa hiyo wamewadharau watu wangu, na hawawaoni tena kama taifa. 25Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Kama sijathibitisha agano langu na usiku na mchana, na kuziweka wakfu sheria za mbingu na nchi, 26basi nitawakataa wazao wa Yakobo na Daudi mtumishi wangu, na sitachagua mmoja wa wanawe kutawala wazao wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Kwa maana nitawarudisha kutoka nchi ya kutekwa kwao na kuwaonea huruma.’ ”
Iliyochaguliwa sasa
Yeremia 33: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.