Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 32

32
Yeremia anunua shamba
1Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, katika mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Nebukadneza. 2Wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli lilikuwa limeuzingira mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ua wa walinzi katika jumba la kifalme la Yuda.
3Basi Sedekia mfalme wa Yuda alikuwa amemfunga huko akisema, “Kwa nini unatabiri hivyo? Wewe unasema, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Ninakaribia kuutia mji huu mkononi mwa mfalme wa Babeli, naye atauteka. 4Sedekia mfalme wa Yuda hataweza kuponyoka mikononi mwa Wakaldayo, lakini kwa hakika atatiwa mikononi mwa mfalme wa Babeli, naye atazungumza naye ana kwa ana na kumwona kwa macho yake mwenyewe. 5Atamchukua Sedekia hadi Babeli, mahali atakapoishi hadi nitakapomshughulikia, asema Mwenyezi Mungu. Kama utapigana dhidi ya Wakaldayo, hutashinda.’ ”
6Yeremia akasema, “Neno la Mwenyezi Mungu lilinijia kusema: 7Hanameli mwana wa Shalumu mjomba wako atakuja kwako na kusema, ‘Nunua shamba langu huko Anathothi, kwa sababu wewe kama jamaa ya karibu ni haki na wajibu wako kulikomboa.’
8“Kisha, kama Mwenyezi Mungu alivyosema, binamu yangu Hanameli alinijia katika ua wa walinzi na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini. Kwa kuwa ni haki yako kulikomboa na kulimiliki, jinunulie.’
“Nilijua kwamba hili lilikuwa neno la Mwenyezi Mungu. 9Hivyo nikalinunua shamba hilo lililoko Anathothi kutoka kwa binamu yangu Hanameli, nami nikampimia shekeli kumi na saba#32:9 Shekeli 17 ni sawa na gramu 200. za fedha. 10Nikatia sahihi na kuweka muhuri hati ya kumiliki, nikaweka mashahidi, na kupima ile fedha kwenye mizani. 11Nikachukua ile hati ya kununulia, nakala iliyotiwa muhuri yenye makubaliano na masharti, pia pamoja na ile nakala isiyo na muhuri, 12nami nikampa Baruku mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, hati hii mbele ya binamu yangu Hanameli, na mbele ya mashahidi waliokuwa wameweka sahihi kwenye hati hii na mbele ya Wayahudi wote waliokuwa wameketi katika ua wa walinzi.
13“Nilimpa Baruku maelezo haya mbele yao: 14‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Chukua hati hizi, yaani nakala zote zenye muhuri na zisizo na muhuri za hati ya kununulia, na uziweke kwenye gudulia la udongo wa mfinyanzi ili zidumu kwa muda mrefu. 15Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Nyumba, mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.’
16“Baada ya kumkabidhi Baruku mwana wa Neria hii hati ya kununulia, nilimwomba Mwenyezi Mungu:
17“Ee Bwana Mungu Mwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza. 18Wewe huonesha upendo kwa maelfu, lakini huleta adhabu kwa ajili ya dhambi za baba mapajani mwa watoto wao baada yao. Ee Mungu mkuu na mwenye uweza, ambaye jina lako ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, 19mashauri yako ni makuu, na matendo yako ni yenye uwezo. Macho yako yanaona njia zote za wanadamu, nawe humlipa kila mmoja kulingana na mwenendo wake, na kwa kadri ya matendo yake. 20Ulitenda ishara za miujiza na maajabu huko Misri, na unafanya hivyo hadi leo, katika Israeli na miongoni mwa wanadamu wote, nawe umejulikana na kufahamika hivyo hadi leo. 21Uliwatoa watu wako Israeli kutoka Misri kwa ishara na maajabu, kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa na kwa utisho mkuu. 22Uliwapa nchi hii uliyokuwa umeapa kuwapa baba zao, nchi inayotiririka maziwa na asali. 23Waliingia na kuimiliki, lakini hawakukutii wala kuifuata sheria yako. Hawakufanya kile ulichowaamuru kufanya. Hivyo ukaleta maafa haya yote juu yao.
24“Tazama jinsi jeshi lilivyouzingira mji huu ili kuuteka. Kwa sababu ya upanga, njaa, na tauni, mji utatiwa mkononi mwa Wakaldayo wanaoushambulia. Ulilolisema limetokea kama unavyoona. 25Ingawa mji utatiwa mikononi mwa Wakaldayo, wewe, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, uliniambia, ‘Nunua shamba kwa fedha mbele ya mashahidi.’ ”
26Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yeremia kusema: 27“Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wa wote wenye mwili. Je, kuna jambo lolote lililo gumu nisiloliweza? 28Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Ninakaribia kuutia mji huu mikononi mwa Wakaldayo, na mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli ambaye atauteka. 29Wakaldayo ambao wanaushambulia mji huu watakuja na kuuchoma moto na kuuteketeza, pamoja na nyumba ambamo watu wamenikasirisha kwa kumfukizia Baali uvumba katika mapaa na kumimina sadaka za vinywaji kwa miungu mingine.
30“Watu wa Israeli na wa Yuda hawakufanya kitu kingine ila uovu mbele zangu tangu ujana wao. Naam, watu wa Israeli hawakufanya kitu kingine ila kunikasirisha kwa kazi ambazo mikono yao imetengeneza, asema Mwenyezi Mungu. 31Tangu siku ulipojengwa hadi sasa, mji huu umenikasirisha na kunighadhibisha kiasi kwamba ni lazima niuondoe machoni pangu. 32Watu wa Israeli na wa Yuda wamenikasirisha kwa uovu wote waliofanya: wao, wafalme wao na maafisa wao, makuhani wao na manabii wao, watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu. 33Walinigeuzia visogo vyao, wala si nyuso zao. Ingawa niliwafundisha tena na tena, hawakupenda kusikiliza wala kuitikia adhabu. 34Waliweka miungu yao ya kuchukiza sana katika nyumba iitwayo kwa Jina langu na kuinajisi. 35Wakajenga mahali pa juu pa kuabudia Baali katika Bonde la Ben-Hinomu, ambapo waliwatoa kafara watoto wao wa kiume na wa kike kwa Moleki, ingawa kamwe sikuwaamuru, wala sikuwaza kwamba watafanya chukizo kama hilo na kumfanya Yuda atende dhambi.
36“Mnasema kuhusu mji huu, ‘Kwa upanga, njaa na tauni, mji utatiwa mkononi mwa mfalme wa Babeli,’ lakini hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: 37Hakika nitawakusanya kutoka nchi zote nilizowafukuzia katika hasira yangu kali na ghadhabu yangu kuu, nitawarudisha mahali hapa na kuwaruhusu waishi salama. 38Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. 39Nitawapa moyo mmoja na kutenda pamoja, ili waniche daima kwa mema yao wenyewe na kwa mema ya watoto wao baada yao. 40Nitafanya nao agano la milele: Kamwe sitaacha kuwatendea mema, nami nitawavuvia kunicha mimi, ili wasinigeuke. 41Nitafurahia kuwatendea mema, na kwa hakika nitawapanda katika nchi hii kwa moyo wangu wote na roho yangu yote.
42“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Kama nilivyoleta maafa haya makubwa kwa watu hawa, ndivyo nitakavyowapa mafanikio niliyowaahidi. 43Kwa mara nyingine tena mashamba yatanunuliwa katika nchi hii ambayo mlisema, ‘Imekuwa ukiwa, isiyo na watu wala wanyama, kwa sababu imetiwa mikononi mwa Wakaldayo.’ 44Mashamba yatanunuliwa kwa fedha, na hati zitatiwa sahihi, zitatiwa muhuri na kushuhudiwa katika nchi ya Benyamini, katika vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu, katika miji ya Yuda na katika miji ya nchi ya vilima, sehemu za magharibi katika miji ya tambarare na katika Negebu, kwa sababu nitarudisha tena mafanikio yao#32:44 au kwa sababu nitawarudisha tena kutoka utumwani, asema Mwenyezi Mungu.”

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 32: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia