Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 31

31
Mahamisho kurudi kwa shangwe
1“Wakati huo, nitakuwa Mungu wa koo zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu,” asema Mwenyezi Mungu.
2Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Watu watakaopona upanga
watapata upendeleo jangwani;
nitakuja niwape Israeli pumziko.”
3Mwenyezi Mungu alitutokea zamani, akisema:
“Nimekupenda kwa upendo wa milele,
nimekuvuta kwa wema.
4Nitakujenga tena, nawe utajengeka upya,
ewe Bikira Israeli.
Utachukua tena matari yako
na kwenda kucheza na wanaofurahi.
5Utapanda tena shamba la mizabibu
juu ya vilima vya Samaria,
wakulima watapanda
na kufurahia matunda yake.
6Siku inakuja ambapo walinzi watapiga kelele
juu ya vilima vya Efraimu, wakisema,
‘Njooni, twendeni juu Sayuni,
kwake Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.’ ”
7Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Mwimbieni Yakobo kwa furaha,
mshangilieni aliye mkuu wa mataifa.
Zifanyeni sifa zenu zisikike, nanyi mseme,
‘Ee Mwenyezi Mungu, okoa watu wako,
mabaki ya Israeli.’
8Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini
na kuwakusanya kutoka miisho ya dunia.
Miongoni mwao watakuwa vipofu na viwete,
mama wajawazito na wenye uchungu wa kuzaa.
Umati mkubwa wa watu watarudi.
9Watakuja wakilia;
wataomba wakati ninawarudisha.
Nitawaongoza kando ya vijito vya maji,
katika njia iliyonyooka hawatajikwaa,
kwa sababu mimi ndimi baba wa Israeli,
naye Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza.
10“Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi mataifa,
litangazeni katika nchi za pwani ya mbali:
‘Yeye aliyewatawanya Israeli atawakusanya
na atalichunga kundi lake la kondoo kama mchungaji.’
11Mwenyezi Mungu atamlipia fidia Yakobo
na kuwakomboa mkononi mwa walio na nguvu kuliko wao.
12Watakuja na kupiga kelele kwa furaha katika miinuko ya Sayuni;
watashangilia ukarimu wa Mwenyezi Mungu:
nafaka, divai mpya na mafuta,
wana-kondoo wachanga
na ndama wa makundi ya ng’ombe nitakaowapa.
Watakuwa kama bustani iliyoneshewa vizuri,
wala hawatahuzunika tena.
13Kisha wanawali watacheza na kufurahi,
vijana wa kiume na wazee pia.
Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha,
nitawapa faraja na furaha badala ya huzuni.
14Nitawashibisha makuhani kwa wingi,
nao watu wangu watajazwa kwa ukarimu wangu,”
asema Mwenyezi Mungu.
15Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Sauti imesikika huko Rama,
maombolezo na kilio kikubwa,
Raheli akiwalilia watoto wake
na anakataa kufarijiwa,
kwa sababu watoto wake hawako tena.”
16Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Izuie sauti yako kulia,
na macho yako yasitoe machozi,
kwa kuwa kazi yako itapata thawabu,”
asema Mwenyezi Mungu.
“Watarudi kutoka nchi ya adui.
17Kwa hiyo kuna tumaini kwa siku zijazo,”
asema Mwenyezi Mungu.
“Watoto wako watarudi nchi yao yenyewe.
18“Hakika nimeyasikia maombolezo ya Efraimu:
‘Ulinirudi kama ndama mkaidi,
nami nimekubali kutii.
Unirudishe, nami nitarudi,
kwa sababu wewe ndiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wangu.
19Baada ya kupotea, nilitubu;
baada ya kuelewa, nilijipiga kifua.
Niliaibika na kuona haya
kwa sababu niliibeba aibu ya ujana wangu.’
20Je, Efraimu si mwanangu mpendwa,
mtoto ninayependezwa naye?
Ingawa mara kwa mara ninanena dhidi yake,
bado ninamkumbuka.
Kwa hiyo moyo wangu unamwonea shauku,
nina huruma kubwa kwa ajili yake,”
asema Mwenyezi Mungu.
21“Weka alama za barabara,
weka vibao vya kuelekeza.
Zingatia vyema njia kuu,
barabara ile unayoipita.
Rudi, ee Bikira Israeli,
rudi kwenye miji yako.
22Utatangatanga hata lini,
ee binti usiye mwaminifu?
Mwenyezi Mungu ameumba kitu kipya duniani:
mwanamke atamlinda mwanaume.”
23Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo, “Nitakapowarudisha toka nchi ya kutekwa kwenu, watu walio katika nchi ya Yuda na miji yake kwa mara nyingine tena watatumia maneno haya: ‘Mwenyezi Mungu akubariki, ee makao ya haki, ee mlima mtakatifu.’ 24Watu wataishi pamoja katika Yuda na miji yake yote, wakulima na wote wanaohamahama na mifugo yao. 25Nitawaburudisha waliochoka na kuwatuliza walio na huzuni.”
26Kwa jambo hili niliamka na kuangalia pande zote. Usingizi wangu ulikuwa mtamu kwangu.
27Mwenyezi Mungu asema, “Siku zinakuja, nitakapoongeza idadi ya watu, na kuzidisha hesabu ya mifugo katika nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda. 28Kama vile nilivyowaangalia ili kung’oa na kubomoa, kuharibu, kuangamiza na kuleta maafa juu yao, vivyo hivyo nitawaangalia ili kujenga na kupanda,” asema Mwenyezi Mungu. 29“Katika siku hizo, watu hawatasema tena,
“ ‘Baba wamekula zabibu chachu,
nayo meno ya watoto yakatiwa ganzi.’
30Badala yake, kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe; yeyote alaye zabibu chachu, meno yake mwenyewe yatatiwa ganzi.
31“Siku zinakuja,” asema Mwenyezi Mungu,
“nitakapofanya agano jipya
na nyumba ya Israeli
na nyumba ya Yuda.
32Halitafanana na agano
nililofanya na baba zao
wakati nilipowashika mkono
kuwaongoza watoke Misri,
kwa sababu walivunja agano langu,
ijapokuwa nilikuwa mume kwao,”
asema Mwenyezi Mungu.
33“Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli
baada ya siku zile,” asema Mwenyezi Mungu.
“Nitaweka sheria yangu katika nia zao,
na kuiandika mioyoni mwao.
Nitakuwa Mungu wao,
nao watakuwa watu wangu.
34Mtu hatamfundisha tena jirani yake,
wala mtu kumfundisha ndugu yake, akisema,
‘Mjue Mwenyezi Mungu,’
kwa sababu wote watanijua mimi,
kuanzia aliye mdogo hata aliye mkubwa kuliko wote,”
asema Mwenyezi Mungu.
“Nitasamehe uovu wao, wala sitazikumbuka dhambi zao tena.”
35Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu,
yeye aliyefanya jua
liwake mchana,
yeye anayeamuru mwezi na nyota
kung’aa usiku,
yeye anayeichafua bahari
ili mawimbi yake yangurume;
Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni
ndilo jina lake:
36“Ikiwa amri hizi zitaondoka machoni pangu,”
asema Mwenyezi Mungu,
“ndipo wazao wa Israeli watakoma
kuwa taifa mbele yangu daima.”
37Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Ikiwa mbingu zilizo juu zitaweza kupimika
na misingi ya dunia chini
ikaweza kuchunguzwa,
ndipo nitakapowakataa wazao wote wa Israeli
kwa sababu ya yote waliyoyatenda,”
asema Mwenyezi Mungu.
38“Siku zinakuja,” asema Mwenyezi Mungu, “mji huu utakapojengwa upya kwa ajili yangu, kuanzia mnara wa Hananeli hadi Lango la Pembeni. 39Kamba ya kupimia itaanzia hapo kuendelea hadi kwenye kilima cha Garebu, na kisha kugeuka kuelekea Goa, 40wanakotupa maiti na majivu, na maeneo yote kuanzia Bonde la Kidroni upande wa mashariki hadi pembe ya Lango la Farasi patakuwa mahali patakatifu kwa Mwenyezi Mungu. Mji huu kamwe hautang’olewa wala kubomolewa tena.”

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 31: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia