Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 36

36
Yehoyakimu achoma kitabu cha Yeremia
1Katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilimjia nabii Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kusema: 2“Chukua kitabu uandike ndani yake maneno yote niliyonena nawe kuhusu Israeli, Yuda na mataifa mengine yote, tangu nilipoanza kunena nawe wakati wa utawala wa Yosia hadi sasa. 3Labda watu wa Yuda watakaposikia maafa ninayokusudia kuwapiga nayo, kila mmoja wao atageuka kutoka njia zake mbaya, kisha nitasamehe uovu wao na dhambi yao.”
4Hivyo Yeremia akamwita Baruku mwana wa Neria, naye Yeremia alipokuwa akiyakariri maneno yote aliyoyasema Mwenyezi Mungu, Baruku akayaandika katika kitabu. 5Kisha Yeremia akamwambia Baruku, “Nimezuiliwa; mimi siwezi kuingia katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. 6Basi wewe nenda katika nyumba ya Mwenyezi Mungu siku ya kufunga, uwasomee watu maneno ya Mwenyezi Mungu kutoka kitabu hiki yale uliyoyaandika kutoka kinywani mwangu. Wasomee watu wote wa Yuda waliofika kutoka miji yao. 7Labda wataomba na kusihi mbele za Mwenyezi Mungu na kila mmoja akageuka kutoka njia zake mbaya, kwa sababu hasira na ghadhabu zilizotamkwa dhidi ya watu hawa na Mwenyezi Mungu ni kubwa.”
8Baruku mwana wa Neria akafanya kila kitu nabii Yeremia alichomwambia kufanya. Alisoma maneno ya Mwenyezi Mungu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu kutoka kile kitabu. 9Katika mwezi wa tisa wa mwaka wa tano wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, wakati wa kufunga mbele za Mwenyezi Mungu, ilitangazwa kwa watu wote waliokuwa Yerusalemu, na wale wote waliokuwa wamekuja kutoka miji ya Yuda. 10Kutoka chumba cha Gemaria mwana wa Shafani mwandishi, kilichokuwa katika ua wa juu kwenye ingilio la Lango Jipya la Hekalu, Baruku akawasomea watu wote waliokuwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu maneno ya Yeremia katika kile kitabu.
11Basi Mikaya mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya Mwenyezi Mungu kutoka kile kitabu, 12alishuka hadi chumba cha mwandishi kwenye jumba la kifalme, mahali walipokuwa wameketi maafisa wote: yaani Elishama mwandishi, Delaya mwana wa Shemaya, Elnathani mwana wa Akbori, Gemaria mwana wa Shafani, Sedekia mwana wa Hanania, na maafisa wengine wote. 13Baada ya Mikaya kuwaambia kila kitu ambacho alikuwa amesikia Baruku akiwasomea watu katika kile kitabu, 14maafisa wote wakamtuma Yehudi mwana wa Nethania, mwana wa Shelemia, mwana wa Kushi, kumwambia Baruku, “Leta hicho kitabu ambacho umewasomea watu, nawe mwenyewe uje.” Ndipo Baruku mwana wa Neria akawaendea akiwa na hicho kitabu mkononi mwake. 15Wakamwambia, “Tafadhali, keti na utusomee hicho kitabu.”
Ndipo Baruku akawasomea kile kitabu. 16Walipoyasikia maneno hayo yote, wakatazamana wao kwa wao kwa woga na kumwambia Baruku, “Lazima tutoe taarifa ya maneno haya yote kwa mfalme.” 17Kisha wakamuuliza Baruku, “Tuambie, uliandikaje haya yote? Je, yalitoka kinywani mwa Yeremia?”
18Baruku akajibu, “Ndiyo, maneno haya yote yalitoka kinywani mwa Yeremia, nami nikayaandika kwa wino katika hiki kitabu.”
19Ndipo wale maafisa wakamwambia Baruku, “Wewe na Yeremia nendeni mkajifiche. Mtu yeyote asijue mahali mlipo.”
20Baada ya kuhifadhi kile kitabu ndani ya chumba cha Elishama mwandishi, wakamwendea mfalme katika ua wa nje na kumwarifu kila kitu. 21Mfalme akamtuma Yehudi akachukue kile kitabu. Yehudi akakileta hicho kitabu kutoka chumba cha Elishama mwandishi, na akakisoma mbele ya mfalme na maafisa wakiwa wamesimama kando ya mfalme. 22Ulikuwa mwezi wa tisa, na mfalme alikuwa ameketi chumba cha wakati wa baridi akiota moto. 23Hata ikawa kila wakati Yehudi alipomaliza kusoma kurasa tatu au nne za hicho kitabu, mfalme alizikata kwa kisu cha mwandishi na kuzitupia motoni, hadi kitabu chote kikateketea. 24Mfalme na watumishi wake wote waliosikia yote yaliyosomwa hawakuonesha hofu yoyote, wala hawakuyararua mavazi yao. 25Hata ingawa Elnathani, Delaya na Gemaria walimsihi mfalme asikichome kile kitabu, yeye hakuwasikiliza. 26Badala yake, mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, Seraya mwana wa Azrieli, na Shelemia mwana wa Abdeeli kuwakamata mwandishi Baruku na nabii Yeremia. Lakini Mwenyezi Mungu alikuwa amewaficha.
27Baada ya mfalme kuchoma kile kitabu kilichokuwa na yale maneno Baruku aliyokuwa ameyaandika kutoka kinywani mwa Yeremia, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Yeremia likisema: 28“Chukua kitabu kingine na uandike juu yake maneno yote yaliyokuwa katika kile kitabu cha kwanza, ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda amekiteketeza kwa moto. 29Mwambie pia Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Ulikiteketeza kile kitabu ukasema, “Kwa nini uliandika kwenye kitabu kwamba kwa hakika mfalme wa Babeli angekuja na kuangamiza nchi hii, na kuwakatilia mbali watu na wanyama kutoka humo?” 30Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu Yehoyakimu mfalme wa Yuda: Hatakuwa na mtu yeyote atakayekalia kiti cha utawala cha Daudi; maiti yake itatupwa nje kwenye joto wakati wa mchana na kupigwa na baridi wakati wa usiku. 31Nitamwadhibu yeye, watoto wake na watumishi wake kwa ajili ya uovu wao. Nitaleta juu yao na wote wanaoishi Yerusalemu na watu wa Yuda kila maafa niliyoyasema dhidi yao, kwa sababu hawajasikiliza.’ ”
32Kisha Yeremia akachukua kitabu kingine na kumpa mwandishi Baruku mwana wa Neria, naye kama Yeremia alivyosema, Baruku akaandika juu yake maneno yote ya kile kitabu ambacho Yehoyakimu mfalme wa Yuda alikuwa amekichoma moto, na maneno mengine mengi yaliyofanana na hayo yaliyoongezewa humo.

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 36: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia