Isaya 55
55
Mwaliko kwa wenye kiu
1“Haya! Njooni, ninyi nyote wenye kiu,
njooni kwenye maji;
nanyi ambao hamna fedha,
njooni, nunueni na mle!
Njooni, nunueni divai na maziwa
bila fedha na bila gharama.
2Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula,
na kutaabikia kitu kisichoshibisha?
Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri,
nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono.
3Tegeni sikio mje kwangu,
nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi.
Nitafanya agano la milele nanyi,
pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi.
4Tazama, nimemfanya kuwa shahidi wa mataifa,
kiongozi na jemadari wa mataifa.
5Hakika utaita mataifa usiyoyajua,
nayo mataifa yale yasiyokujua yataharakisha kukujia,
kwa sababu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli,
kwa maana amekutukuza.”
6Mtafuteni Mwenyezi Mungu maadamu anapatikana;
mwiteni maadamu yu karibu.
7Mtu mwovu na aiache njia yake,
na mtu mbaya na ayaache mawazo yake.
Yeye na amrudie Mwenyezi Mungu, naye atamrehemu,
arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.
8“Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu,
wala njia zenu si njia zangu,”
asema Mwenyezi Mungu.
9“Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia,
ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu
na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.
10Kama vile mvua na theluji
ishukavyo kutoka mbinguni,
nayo hairudi tena huko
bila kunywesha dunia
na kuichipusha na kuistawisha,
ili itoe mbegu kwa mpanzi
na mkate kwa mlaji,
11ndivyo lilivyo neno langu litokalo kinywani mwangu:
Halitanirudia tupu,
bali litatimiliza lile nililokusudia,
na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma.
12Mtatoka nje kwa furaha
na kuongozwa kwa amani;
milima na vilima
vitapaza sauti kwa nyimbo mbele yenu,
nayo miti yote ya shambani
itapiga makofi.
13Badala ya kichaka cha miiba
itaota miti ya misunobari,
na badala ya michongoma
utaota mhadasi.
Hili litakuwa jambo la kumpatia Mwenyezi Mungu jina,
kwa ajili ya ishara ya milele,
ambayo haitaharibiwa.”
Iliyochaguliwa sasa
Isaya 55: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.