Isaya 56
56
Wokovu kwa wengine
1Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Dumisheni haki
na mkatende lile lililo sawa,
kwa maana wokovu wangu u karibu
na haki yangu itafunuliwa upesi.
2Amebarikiwa mtu yule atendaye hili,
mtu yule alishikaye kwa uthabiti,
yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi,
auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.”
3Usimwache mgeni aambatanaye na Mwenyezi Mungu aseme,
“Hakika Mwenyezi Mungu atanitenga na watu wake.”
Usimwache towashi yeyote alalamike akisema,
“Mimi ni mti mkavu tu.”
4Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Kwa matowashi washikao Sabato zangu,
ambao huchagua kile kinachonipendeza
na kulishika sana agano langu:
5hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake
kumbukumbu na jina bora
kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike:
nitawapa jina lidumulo milele,
ambalo halitakatiliwa mbali.
6Wageni wanaoambatana na Mwenyezi Mungu
ili kumtumikia,
kulipenda jina la Mwenyezi Mungu,
na kumwabudu yeye,
wote washikao Sabato bila kuinajisi
na ambao hushika sana agano langu:
7hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu
na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala.
Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao
zitakubalika juu ya madhabahu yangu;
kwa maana nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala kwa mataifa yote.”
8Bwana Mungu Mwenyezi asema, yeye awakusanyaye
Waisraeli waliohamishwa:
“Bado nitawakusanya wengine kwao
zaidi ya hao ambao wamekusanywa tayari.”
Mashtaka ya Mwenyezi Mungu dhidi ya waovu
9Njooni, enyi wanyama wote wa kondeni,
njooni mle, ninyi wanyama wote wa mwituni!
10Walinzi wa Israeli ni vipofu,
wote wamepungukiwa na maarifa;
wote ni mbwa walio bubu,
hawawezi kubweka;
hulala na kuota ndoto,
hupenda kulala.
11Ni mbwa wenye tamaa kubwa,
kamwe hawatosheki.
Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu;
wote wamegeukia njia yao wenyewe,
kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe.
12Kila mmoja hulia, “Njooni, tupate mvinyo!
Tunywe kileo sana!
Kesho itakuwa kama leo,
au hata bora zaidi.”
Iliyochaguliwa sasa
Isaya 56: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.