Isaya 2:1-11
Isaya 2:1-11 NENO
Hili ndilo aliloliona Isaya mwana wa Amozi kuhusu Yuda na Yerusalemu: Katika siku za mwisho mlima wa Hekalu la Mwenyezi Mungu utaimarishwa kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote, utainuliwa juu ya vilima, na mataifa yote yatamiminika huko. Mataifa mengi yatakuja na kusema, “Njooni, twendeni kwenye mlima wa Mwenyezi Mungu, kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo. Atatufundisha njia zake, ili tuweze kuenenda katika mapito yake.” Torati itatoka Sayuni, neno la Mwenyezi Mungu litatoka Yerusalemu. Atahukumu kati ya mataifa na ataamua migogoro ya mataifa mengi. Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine, wala hawatajifunza vita tena. Njooni, enyi nyumba ya Yakobo, tutembeeni katika nuru ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu umewatelekeza watu wako, nyumba ya Yakobo. Wamejaa ushirikina unaotoka Mashariki, wanapiga ramli kama Wafilisti na wanashikana mikono na wapagani. Nchi yao imejaa fedha na dhahabu, hakuna mwisho wa hazina zao. Nchi yao imejaa farasi, hakuna mwisho wa magari yao ya vita. Nchi yao imejaa sanamu; wanasujudia kazi za mikono yao, vitu vile vidole vyao vimevitengeneza. Kwa hiyo mwanadamu atashushwa na binadamu atanyenyekezwa: usiwasamehe. Ingieni kwenye miamba, jificheni ardhini kutokana na utisho wa Mwenyezi Mungu na utukufu wa enzi yake! Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa na kiburi cha wanadamu kitashushwa, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.