Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 2

2
Mlima wa Mwenyezi Mungu
(Mika 4:1-3)
1Hili ndilo aliloliona Isaya mwana wa Amozi kuhusu Yuda na Yerusalemu:
2Katika siku za mwisho
mlima wa Hekalu la Mwenyezi Mungu utaimarishwa
kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote,
utainuliwa juu ya vilima,
na mataifa yote yatamiminika huko.
3Mataifa mengi yatakuja na kusema,
“Njooni, twendeni kwenye mlima wa Mwenyezi Mungu,
kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.
Atatufundisha njia zake,
ili tuweze kuenenda katika mapito yake.”
Torati itatoka Sayuni,
neno la Mwenyezi Mungu litatoka Yerusalemu.
4Atahukumu kati ya mataifa
na ataamua migogoro ya mataifa mengi.
Watafua panga zao ziwe majembe,
na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi.
Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine,
wala hawatajifunza vita tena.
5Njooni, enyi nyumba ya Yakobo,
tutembeeni katika nuru ya Mwenyezi Mungu.
Siku ya Mwenyezi Mungu
6Mwenyezi Mungu umewatelekeza watu wako,
nyumba ya Yakobo.
Wamejaa ushirikina unaotoka Mashariki,
wanapiga ramli kama Wafilisti
na wanashikana mikono na wapagani.
7Nchi yao imejaa fedha na dhahabu,
hakuna mwisho wa hazina zao.
Nchi yao imejaa farasi,
hakuna mwisho wa magari yao ya vita.
8Nchi yao imejaa sanamu;
wanasujudia kazi za mikono yao,
vitu vile vidole vyao vimevitengeneza.
9Kwa hiyo mwanadamu atashushwa
na binadamu atanyenyekezwa:
usiwasamehe.
10Ingieni kwenye miamba,
jificheni ardhini
kutokana na utisho wa Mwenyezi Mungu
na utukufu wa enzi yake!
11Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa
na kiburi cha wanadamu kitashushwa,
Mwenyezi Mungu peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.
12Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anayo siku aliyoiweka akiba
kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi,
kwa wote wanaojikweza
(nao watanyenyekezwa),
13kwa mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu sana,
na mialoni yote ya Bashani,
14kwa milima yote mirefu
na vilima vyote vilivyoinuka,
15kwa kila mnara ulio mrefu sana
na kila ukuta wenye ngome,
16kwa kila meli ya biashara#2:16 au ya Tarshishi (taz. 1 Wafalme 10:22; 22:48; 2 Nyakati 9:21; 20:36; Isaya 60:9).,
na kila mashua ya kifahari.
17Majivuno ya mwanadamu yatashushwa,
na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa,
Mwenyezi Mungu peke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo,
18nazo sanamu zitatoweka kabisa.
19Watu watakimbilia kwenye mapango ndani ya miamba,
na kwenye mahandaki ardhini
kutokana na utisho wa Mwenyezi Mungu
na utukufu wa enzi yake,
ainukapo kuitikisa dunia.
20Siku ile, watu watawatupia
panya na popo
sanamu zao za fedha na za dhahabu,
walizozitengeneza ili waziabudu.
21Watakimbilia kwenye mapango miambani
na kwenye nyufa za miamba
kutokana na utisho wa Mwenyezi Mungu
na utukufu wa enzi yake,
ainukapo kuitikisa dunia.
22Acheni kumtumainia mwanadamu,
ambaye hana kitu ila pumzi katika pua zake.
Yeye ana thamani gani?

Iliyochaguliwa sasa

Isaya 2: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia