Isa 2:1-11
Isa 2:1-11 SUV
Hili ni neno aliloliona Isaya mwana wa Amozi katika habari za Yuda na Yerusalemu. Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya BWANA utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa BWANA, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la BWANA katika Yerusalemu. Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya BWANA. Maana wewe umewaacha watu wako, nyumba ya Israeli, kwa sababu wamejaa kawaida za mashariki, nao ni wapiga ramli kama Wafilisti, na wanapana mikono na wana wa wageni. Tena nchi yao imejaa fedha na dhahabu, wala hapana mwisho wa hazina zao; tena nchi yao imejaa farasi, wala hapana mwisho wa magari yao. Tena nchi yao imejaa sanamu; huabudu kazi ya mikono yao, vitu vilivyofanywa kwa vidole vyao wenyewe. Mtu mnyonge huinama, na mtu mkubwa hujidhili; kwa hiyo usiwasamehe. Ingia ndani ya jabali; ukajifiche mavumbini mbele za utisho wa BWANA, mbele za utukufu wa enzi yake. Macho ya mwanadamu yaliyoinuka yatashushwa chini, na kiburi cha mwanadamu kitainamishwa, naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo.