Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waebrania 6

6
Hatari ya kuanguka
1Kwa hiyo, tukiachana na mafundisho yale ya awali kuhusu Al-Masihi na tukisonga mbele ili tufikie utimilifu, tusiweke tena msingi wa mafundisho ya kuzitubia kazi zisizo na uhai na imani katika Mungu, 2mafundisho kuhusu aina za ubatizo#6:2 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali. Wafuasi wa Isa Al-Masihi pia wanapokea Roho wa Mungu kama dhibitisho ya imani yao., kuwekea watu mikono, ufufuo wa wafu, na hukumu ya milele. 3Mungu akitujalia tutafanya hivyo.
4Kwa kuwa ni vigumu kwa wale ambao wakati fulani walishapata nuru, ambao walishaonja kipawa cha mbinguni, ambao wamekwisha kushiriki katika Roho wa Mungu, 5ambao wameonja uzuri wa neno la Mungu na nguvu za wakati ujao, 6kisha wakianguka, kuwarejesha tena katika toba. Kwa kuwa wanamsulubisha Mwana wa Mungu#6:6 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili. tena na kumdhalilisha hadharani, nayo ikawa hasara kwao.
7Ardhi inayopokea mvua inayonyesha mara kwa mara juu yake na baadaye inatoa mazao ya kuwanufaisha wale ambao inalimwa kwa ajili yao, hupokea baraka za Mungu. 8Lakini ardhi ikizaa miiba na mibaruti, haina thamani na iko hatarini kulaaniwa. Mwisho wake ni kuchomwa moto.
9Ingawa tunasema hivi, ndugu zangu wapendwa, kwa upande wenu tuna hakika ya mambo mema zaidi, mambo kuhusu wokovu. 10Mungu si mdhalimu: yeye hataisahau kazi yenu na upendo ule mlioonesha kwa ajili yake katika kuwahudumia watakatifu na hata sasa mnaendelea kuwahudumia. 11Nasi twataka kila mmoja wenu aoneshe bidii hiyo hiyo ili mpate kujua uhakika kamili wa lile tumaini hadi mwisho, 12ili msije mkawa wavivu, bali mpate kuwaiga wale ambao kwa imani na saburi hurithi zile ahadi.
Uhakika wa ahadi ya Mwenyezi Mungu
13Mungu alipompa Ibrahimu ahadi yake, kwa sababu hapakuwa mwingine mkuu kuliko yeye ambaye angeapa naye, aliapa kwa nafsi yake, 14akisema, “Hakika nitakubariki na kukupa wazao wengi.”#6:14 Mwanzo 22:17 15Ibrahimu naye, baada ya kungoja kwa saburi, alipokea kile kilichoahidiwa.
16Wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao, nacho kiapo hicho huthibitisha kile kilichosemwa na hivyo humaliza mabishano yote. 17Mungu alipotaka kuonesha kwa udhahiri zaidi ile asili ya kutokubadilika kwa ahadi yake kwa warithi wa ahadi, aliithitibisha kwa kiapo. 18Mungu alifanya hivyo ili kwa vitu viwili visivyobadilika, yaani ahadi yake na kiapo chake, ambavyo kwavyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi ambao tumemkimbilia ili tulishike lile tumaini lililowekwa mbele yetu tuwe na faraja thabiti. 19Tunalo tumaini hili kama nanga ya roho iliyo imara na thabiti. Tumaini hili huingia katika mahali patakatifu nyuma ya pazia, 20ambapo Isa mtangulizi wetu aliingia kwa niaba yetu. Yeye amekuwa Kuhani Mkuu milele, kwa mfano wa Melkizedeki.

Iliyochaguliwa sasa

Waebrania 6: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia