Waebrania 5
5
1Kwa maana kila kuhani mkuu anayechaguliwa miongoni mwa wanadamu anawekwa kuwawakilisha kwa mambo yanayomhusu Mungu, ili apate kutoa matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi. 2Kwa kuwa yeye mwenyewe ni dhaifu, aweza kuwachukulia kwa upole wale wasiojua na kupotoka. 3Hii ndiyo sababu inampasa kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe na vivyo hivyo kwa ajili ya dhambi za watu. 4Hakuna anayejitwalia heshima hii mwenyewe; ni lazima aitwe na Mungu, kama vile Haruni alivyoitwa.
5Pia Al-Masihi hakujitwalia utukufu yeye mwenyewe wa kuwa Kuhani Mkuu, bali Mungu alimwambia,
“Wewe ni Mwanangu;
leo mimi nimekuwa Baba yako.”#5:5 Zaburi 2:7
6Pia mahali pengine asema,
“Wewe ni kuhani milele,
kwa mfano wa Melkizedeki.”#5:6 Zaburi 110:4
7Katika siku za maisha ya Isa hapa duniani, alimtolea maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, yeye awezaye kumwokoa na mauti, naye Mungu akamsikia kwa sababu ya kutii kwake kwa unyenyekevu. 8Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza utiifu kutokana na mateso aliyoyapata, 9naye akiisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii. 10Naye amewekwa na Mungu kuwa Kuhani Mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.
Wito wa kukua kiroho
11Tunayo mengi ya kusema kuhusu habari ya ukuhani huu, lakini ni vigumu kuyaeleza, kwa sababu ninyi ni wazito wa kuelewa. 12Kwa hakika, ingawa hadi wakati huu ingewapasa kuwa walimu, bado mnahitaji mtu wa kuwafundisha tena hatua za awali za kweli ya neno la Mungu. Mnahitaji maziwa, wala si chakula kigumu! 13Kwa maana yeyote aishiye kwa kunywa maziwa bado yeye ni mtoto mchanga, hana ujuzi katika mafundisho kuhusu neno la haki. 14Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu wazima, ambao kwa kujizoeza wamejifunza kupambanua kati ya mema na mabaya.
Iliyochaguliwa sasa
Waebrania 5: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.