Waebrania 7
7
Kuhani Melkizedeki
1Kwa kuwa huyu Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana. Alipokutana na Ibrahimu akirudi kutoka kuwashinda wafalme, Melkizedeki alimbariki, 2naye Ibrahimu alimpa sehemu ya kumi ya kila kitu. Kwanza, jina hilo Melkizedeki maana yake ni “mfalme wa haki”. Na pia “mfalme wa Salemu” maana yake ni “mfalme wa amani”. 3Hana baba wala mama, hana ukoo, hana mwanzo wala mwisho wa siku zake, kama Mwana wa Mungu. Yeye adumu akiwa kuhani milele.
4Tazama jinsi alivyokuwa mkuu: Hata Ibrahimu, baba yetu wa zamani, alimpa sehemu ya kumi ya nyara zake. 5Basi sheria inawaagiza wana wa Lawi ambao hufanyika makuhani kupokea sehemu ya kumi kutoka kwa watu ambao ni ndugu zao, ingawa ndugu zao ni wazao wa Ibrahimu. 6Huyu Melkizedeki, ingawa hakufuatia ukoo wake kutoka kwa Lawi, lakini alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Ibrahimu na kumbariki yeye aliyekuwa na zile ahadi. 7Wala hakuna shaka kwamba mdogo hubarikiwa na aliye mkuu kuliko yeye. 8Kwa upande mmoja, sehemu ya kumi hupokelewa na watu ambao hufa; lakini kwa upande mwingine hupokelewa na yeye ambaye hushuhudiwa kuwa yu hai. 9Mtu anaweza hata kusema kwamba Lawi, ambaye hupokea sehemu ya kumi, alitoa hiyo sehemu ya kumi kupitia kwa Ibrahimu, 10kwa sababu Melkizedeki alipokutana na Ibrahimu, Lawi alikuwa bado katika viuno vya baba yake wa zamani.
Isa mfano wa Melkizedeki
11Kama ukamilifu ungeweza kupatikana kupitia kwa ukuhani wa Walawi (kwa kuwa katika msingi huo, sheria ilitolewa kwa watu), kwa nini basi kulikuwa na haja ya kuja kuhani mwingine: kuhani kwa mfano wa Melkizedeki, wala si kwa mfano wa Haruni? 12Kwa kuwa ukuhani ukibadilika, lazima sheria nayo ibadilike. 13Yeye ambaye mambo haya yanasemwa alikuwa wa kabila lingine, na hakuna mtu wa kabila hilo aliyewahi kuhudumu katika madhabahu. 14Kwa maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika uzao wa Yuda, tena kuhusu kabila hilo Musa hakusema lolote kwa habari za makuhani. 15Tena hayo tuliyosema yako wazi zaidi kama akitokea kuhani mwingine kama Melkizedeki, 16yeye ambaye amefanyika kuhani si kwa misingi ya sheria kama ilivyokuwa kwa baba zake, bali kwa misingi ya uwezo wa uzima usioharibika. 17Kwa maana imeshuhudiwa kwamba:
“Wewe ni kuhani milele,
kwa mfano wa Melkizedeki.”#7:17 Zaburi 110:4
18Kwa upande mmoja, ile amri ya mwanzo isiyofaa na dhaifu imebatilishwa 19(kwa maana sheria haikufanya kitu chochote kuwa kikamilifu). Kwa upande mwingine, tumeletewa tumaini lililo bora zaidi ambalo linatuleta karibu na Mungu.
20Nalo tumaini hilo halikutolewa pasipo kiapo! Wengine walikuwa makuhani pasipo kiapo chochote, 21lakini Isa alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alimwambia:
“Mwenyezi Mungu ameapa,
naye hatabadilisha mawazo yake:
‘Wewe ni kuhani milele.’#7:21 Zaburi 110:4”
22Kwa ajili ya kiapo hiki, Isa amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi.
23Basi kumekuwa na makuhani wengi wa aina hiyo, kwa kuwa kifo kiliwazuia kuendelea na huduma yao ya ukuhani. 24Lakini kwa sababu Isa anaishi milele, anao ukuhani wa kudumu. 25Kwa hiyo anaweza kuwaokoa kabisa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake, kwa sababu yeye adumu daima kuomba kwa ajili yao.
26Kwa kuwa ilitupasa tuwe na Kuhani Mkuu wa namna hii, yaani aliye mtakatifu, asiye na lawama, asiye na dosari, aliyetengwa na wenye dhambi na kuinuliwa juu ya mbingu. 27Yeye hahitaji kutoa dhabihu siku kwa siku kwa ajili ya dhambi, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu kama wale makuhani wakuu wengine. Yeye alitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zao mara moja tu, alipojitoa mwenyewe. 28Kwa kuwa sheria huwaweka makuhani wakuu watu ambao ni dhaifu; lakini lile neno la kiapo, lililokuja baada ya sheria, lilimweka Mwana, ambaye amefanywa kuwa mkamilifu milele.
Iliyochaguliwa sasa
Waebrania 7: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.