Mwanzo 50
50
1Basi Yusufu akamwangukia baba yake, akalilia juu yake na akambusu. 2Ndipo Yusufu akawaagiza matabibu waliokuwa wakimhudumia, wamtie baba yake Israeli dawa asioze. Hivyo matabibu wakamtia dawa asioze, 3wakatumia siku arobaini, muda uliohitajika kutia dawa asioze. Nao Wamisri wakamwombolezea Yakobo kwa siku sabini.
4Siku za kumwombolezea zilipokwisha, Yusufu akawaambia washauri wa Farao, “Kama nimepata kibali machoni penu semeni na Farao kwa ajili yangu. Mwambieni, 5‘Baba yangu aliniapisha na kuniambia, “Mimi niko karibu kufa; unizike katika kaburi lile nililochimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani.” Sasa nakuomba uniruhusu niende kumzika baba yangu, nami nitarudi.’ ”
6Farao akasema, “Panda, uende kumzika baba yako, kama alivyokuapiza kufanya.”
7Hivyo Yusufu akapanda kwenda kumzika baba yake. Maafisa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, watu mashuhuri wa baraza lake, na watu mashuhuri wote wa Misri. 8Hawa ni mbali na watu wote wa nyumbani mwa Yusufu, na ndugu zake, na wale wote wa nyumbani mwa baba yake. Ni watoto wao, makundi yao ya kondoo, mbuzi na ng’ombe tu waliobakia katika nchi ya Gosheni. 9Magari ya vita na wapanda farasi pia walipanda pamoja naye. Likawa kundi kubwa sana.
10Walipofika kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Atadi, karibu na Yordani, wakalia kwa sauti na kwa uchungu. Yusufu akakaa huko kwa siku saba kumwombolezea baba yake. 11Wakanaani walioishi huko walipoona maombolezo yaliyofanyika katika sakafu ile ya kupuria ya Atadi, wakasema, “Wamisri wanafanya maombolezo makubwa.” Kwa hiyo mahali pale karibu na Yordani pakaitwa Abel-Mizraimu.#50:11 yaani Maombolezo ya Wamisri
12Hivyo wana wa Yakobo wakafanya kama baba yao alivyowaagiza: 13Wakamchukua hadi nchi ya Kanaani, wakamzika kwenye pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre, ambalo Ibrahimu alilinunua kutoka kwa Efroni Mhiti pamoja na shamba liwe mahali pa kuzikia. 14Baada ya Yusufu kumzika baba yake, akarudi Misri pamoja na ndugu zake na wale wote waliokuwa wameenda naye kumzika baba yake.
Yusufu awaondolea ndugu zake mashaka
15Ndugu zake Yusufu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje kama Yusufu ataweka kinyongo dhidi yetu na kutulipa mabaya yote tuliyomtendea?” 16Kwa hiyo wakampelekea Yusufu ujumbe, wakasema, “Kabla baba yako hajafa aliacha maagizo haya: 17‘Hili ndilo mtakalomwambia Yusufu: Ninakuomba uwasamehe ndugu zako dhambi na mabaya kwa vile walivyokutenda vibaya.’ Sasa tafadhali samehe dhambi za watumishi wa Mungu wa baba yako.” Ujumbe huu ulipomfikia, Yusufu akalia.
18Ndipo ndugu zake wakaja na kujitupa chini mbele yake. Wakasema, “Sisi ni watumwa wako.”
19Lakini Yusufu akawaambia, “Msiogope. Je, mimi ni badala ya Mungu? 20Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi. 21Hivyo basi, msiogope. Mimi nitawatunza ninyi nyote pamoja na watoto wenu.” Akawafariji na kusema nao kwa wema.
Kifo cha Yusufu
22Yusufu akakaa katika nchi ya Misri, yeye pamoja na jamaa yote ya baba yake. Akaishi miaka mia moja na kumi, 23naye akaona kizazi cha tatu cha watoto wa Efraimu. Pia akaona watoto wa Makiri mwana wa Manase, wakawekwa magotini mwa Yusufu walipozaliwa.
24Ndipo Yusufu akawaambia ndugu zake, “Mimi ninakaribia kufa. Lakini kwa hakika Mungu atawasaidia na kuwachukueni kutoka nchi hii na kuwapeleka katika nchi aliyomwahidi kwa kiapo Ibrahimu, Isaka na Yakobo.” 25Naye Yusufu akawaapisha wana wa Israeli na kuwaambia, “Hakika Mungu atawasaidia, nanyi ni lazima mhakikishe mmepandisha mifupa yangu kutoka mahali hapa.”
26Kwa hiyo Yusufu akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. Baada ya kumtia dawa asioze, akawekwa kwenye jeneza huko Misri.
Iliyochaguliwa sasa
Mwanzo 50: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.