Kutoka Utangulizi
Utangulizi
Neno “Kutoka” linatokana na neno la Kiyunani “Exodos”, ambalo maana yake ni “Kutoka”, “Kuhama” au “Kuondoka”. Kitabu hiki kilipewa jina hili na watafsiri wa Maandiko Matakatifu kwa Kiyunani lijulikanalo kama “Septuagint” kwa sababu kinaelezea jinsi Waisraeli walivyoongozwa na Mwenyezi Mungu kuondoka nchi ya Misri. Kitabu hiki kinaelezea mambo makubwa aliyoyafanya Mwenyezi Mungu katika kuwaokoa Waisraeli kutoka maisha ya utumwa kule Misri. Huu ulikuwa ni muujiza mkubwa katika historia ya taifa la Israeli.
Kutokana na maisha magumu waliyoishi Waisraeli utumwani huko Misri, Mwenyezi Mungu alimchagua Musa kutekeleza mpango wake maalum wa ukombozi wa watu wake, yaani kuwaondoa utumwani Misri na kuwaongoza hadi nchi ya Kanaani, ambayo aliwaahidi baba zao.
Mwenyezi Mungu alionesha nguvu zake kwa Waisraeli na kwa Wamisri katika yale mapigo kumi. Pigo la mwisho lilisababisha Waisraeli waruhusiwe kuondoka Misri. Kabla ya Waisraeli kuondoka Misri waliadhimisha Sikukuu ya Pasaka. Tukio hili lilifanyika katika historia iliyofuata baadaye na kuandikwa katika vitabu vya Israeli.
Waisraeli walianza safari ya kuondoka Misri wakiwa wanalindwa na kuongozwa na Mwenyezi Mungu kupitia nguzo ya wingu wakati wa mchana, na nguzo ya moto wakati wa usiku. Walipofika Mlima Sinai, Mwenyezi Mungu alifanya Agano lake na Waisraeli kwa kuwapa sheria za kuongoza maisha yao. Hapo Mlima Sinai, Musa alipewa ufunuo mkuu na wa pekee wa jinsi taifa la Israeli lilivyotakiwa kumtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu. Ufunuo huo ndio kiini na asili ya dini ya Kiyahudi.
Mwandishi
Musa.
Kusudi
Kueleza jinsi Mwenyezi Mungu alivyowakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri na kuwafanya kuwa taifa, na kisha kuanza safari ya kwenda Kanaani, nchi aliyowaahidi.
Mahali
Waisraeli wakiwa jangwani, katika Ghuba ya Sinai.
Tarehe
Mnamo 1450–1410 K.K.
Wahusika Wakuu
Musa, Haruni, Miriamu, Farao, Binti Farao, Yethro, Yoshua na Bezaleli.
Wazo Kuu
Kitabu cha Kutoka kinaelezea jinsi Waisraeli walivyoteswa, kunyanyaswa, na kugandamizwa wakiwa utumwani katika nchi ya Misri, kukombolewa kwao kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, kufanyika kwa Agano kati yao na Mwenyezi Mungu, kupewa Torati, kujengwa kwa Hema, na mwanzo wa ukuhani wa Haruni.
Mambo Muhimu
Kutolewa utumwani, na kuanzishwa kwa Pasaka; kuongozwa na Mwenyezi Mungu kuvuka Bahari ya Shamu; kuingia kwenye Agano na Mwenyezi Mungu; kuanzishwa kwa uhusiano baina ya Israeli na Mwenyezi Mungu; kutolewa kwa Amri Kumi katika Mlima Sinai; na Israeli kutambuliwa kuwa taifa takatifu la Mwenyezi Mungu lenye wajibu wa kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa moyo wote na kumtii.
Yaliyomo
Israeli wagandamizwa Misri, na Musa achaguliwa na Mwenyezi Mungu (1:1–4:31)
Ugumu wa Farao na matokeo yake (5:1–11:10)
Kuanzishwa kwa Pasaka na pigo la mwisho (12:1-30)
Kutoka Misri hadi Mlima Sinai (12:31–18:27)
Agano la Mwenyezi Mungu na amri zake (19:1–24:18)
Taratibu za ibada na dhabihu (25:1–40:38).
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka Utangulizi: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.