Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 50:1-13

Mwanzo 50:1-13 NENO

Basi Yusufu akamwangukia baba yake, akalilia juu yake na akambusu. Ndipo Yusufu akawaagiza matabibu waliokuwa wakimhudumia, wamtie baba yake Israeli dawa asioze. Hivyo matabibu wakamtia dawa asioze, wakatumia siku arobaini, muda uliohitajika kutia dawa asioze. Nao Wamisri wakamwombolezea Yakobo kwa siku sabini. Siku za kumwombolezea zilipokwisha, Yusufu akawaambia washauri wa Farao, “Kama nimepata kibali machoni penu semeni na Farao kwa ajili yangu. Mwambieni, ‘Baba yangu aliniapisha na kuniambia, “Mimi niko karibu kufa; unizike katika kaburi lile nililochimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani.” Sasa nakuomba uniruhusu niende kumzika baba yangu, nami nitarudi.’ ” Farao akasema, “Panda, uende kumzika baba yako, kama alivyokuapiza kufanya.” Hivyo Yusufu akapanda kwenda kumzika baba yake. Maafisa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, watu mashuhuri wa baraza lake, na watu mashuhuri wote wa Misri. Hawa ni mbali na watu wote wa nyumbani mwa Yusufu, na ndugu zake, na wale wote wa nyumbani mwa baba yake. Ni watoto wao, makundi yao ya kondoo, mbuzi na ng’ombe tu waliobakia katika nchi ya Gosheni. Magari ya vita na wapanda farasi pia walipanda pamoja naye. Likawa kundi kubwa sana. Walipofika kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Atadi, karibu na Yordani, wakalia kwa sauti na kwa uchungu. Yusufu akakaa huko kwa siku saba kumwombolezea baba yake. Wakanaani walioishi huko walipoona maombolezo yaliyofanyika katika sakafu ile ya kupuria ya Atadi, wakasema, “Wamisri wanafanya maombolezo makubwa.” Kwa hiyo mahali pale karibu na Yordani pakaitwa Abel-Mizraimu. Hivyo wana wa Yakobo wakafanya kama baba yao alivyowaagiza: Wakamchukua hadi nchi ya Kanaani, wakamzika kwenye pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre, ambalo Ibrahimu alilinunua kutoka kwa Efroni Mhiti pamoja na shamba liwe mahali pa kuzikia.