Mwanzo 50:1-13
Mwanzo 50:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo Yosefu akamkumbatia baba yake akilia na kumbusu. Kisha, akawaagiza waganga wake wampake Israeli, baba yake, dawa ili asioze, nao wakafanya hivyo. Kama kawaida, siku arubaini zilihitajika kwa kazi hiyo. Wamisri nao wakaomboleza kifo cha Yakobo kwa muda wa siku sabini. Baada ya matanga kumalizika, Yosefu akawaambia watu wa jamaa ya Farao, “Ikiwa nimekubalika mbele yenu, tafadhali zungumzeni na Farao kwa niaba yangu kwamba baba yangu aliniapisha, akisema, ‘Mimi karibu nitafariki. Yakupasa kunizika katika kaburi nililojichongea katika nchi ya Kanaani.’ Kwa hiyo namwomba aniruhusu niende kumzika baba yangu, kisha nitarudi.” Farao akajibu, “Nenda ukamzike baba yako kama alivyokuapisha.” Basi, Yosefu akaondoka kwenda kumzika baba yake akifuatana na watumishi wote wa Farao, wazee wa nyumba ya Farao, pamoja na wazee wa nchi nzima ya Misri. Hali kadhalika, Yosefu alifuatana na jamaa yake yote, ndugu zake na jamaa yote ya baba yake Yakobo. Katika eneo la Gosheni walibaki watoto wao tu pamoja na kondoo, mbuzi na ng'ombe wao. Pia waliandamana naye wapandafarasi na magari; lilikuwa kundi kubwa sana. Walipofika katika uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, ngambo ya mto Yordani, waliomboleza kwa huzuni kubwa, naye Yosefu akamfanyia baba yake marehemu matanga ya siku saba. Wakanaani wenyeji wa nchi hiyo, walipoyaona maombolezo yaliyofanywa kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, wakasema, “Maombolezo haya ya Wamisri, kweli ni makubwa!” Kwa hiyo, mahali pale pakaitwa Abel-misri, napo pako ngambo ya mto Yordani. Wana wa Yakobo walimfanyia baba yao kama alivyowaagiza: Walimchukua mpaka nchi ya Kanaani, wakamzika katika pango lililokuwa katika shamba kule Makpela, mashariki ya Mamre. Pango pamoja na shamba hilo Abrahamu alikuwa amelinunua kwa Efroni Mhiti, ili pawe mahali pake pa kuzikia.
Mwanzo 50:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yusufu akamwangukia babaye usoni, akamlilila, akambusu. Yusufu akawaagiza watumishi wake waganga wampake baba yake dawa asioze. Waganga wakampaka dawa Israeli. Siku zake arubaini zikaisha, maana siku hizo zilitimiza siku za wale waliohifadhiwa kwa kupakwa dawa. Wamisri wakamwombolezea siku sabini. Siku za kumwombolezea zilipopita, Yusufu alisema na watu wa nyumba ya Farao, akinena, Kama nimeona neema machoni penu, tafadhalini mkaseme masikioni mwa Farao, mkinena, Baba yangu aliniapisha, akisema, Mimi ni katika kufa, unizike katika kaburi langu nililojichimbia katika nchi ya Kanaani. Basi tafadhali uniruhusu niende sasa nikamzike babangu, nami nitarudi. Farao akasema, Nenda, ukamzike baba yako, kama alivyokuapisha. Basi Yusufu akaenda kumzika baba yake, na watumishi wote wa Farao wakaenda pamoja naye, wazee wa nyumbani mwake, na wazee wote wa nchi ya Misri. Na nyumba yote ya Yusufu, na ndugu zake, na nyumba ya baba yake; wakawaacha watoto wao tu, na kondoo wao, na ng'ombe wao, katika nchi ya Gosheni. Kisha wakaenda pamoja naye wapanda farasi, na magari; wakawa jeshi kubwa sana. Wakaja mpaka uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, uliyo ng'ambo ya Yordani. Wakaomboleza huko maombolezo makuu, mazito sana. Akafanya matanga ya baba yake siku saba. Nao waliokaa katika nchi, wale Wakanaani, walipoyaona matanga katika sakafu ya Atadi, wakasema, Matanga haya ya Wamisri ni makuu kwa hiyo mahali pale paliitwa Abel-Misri, iliyo ng'ambo ya Yordani. Wanawe wakamfanyia kama alivyowaagiza; kwa kuwa wanawe wakamchukua mpaka nchi ya Kanaani, na wakamzika katika pango ya shamba la Makpela, iliyo mbele ya Mamre, aliyoinunua Abrahamu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia.
Mwanzo 50:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yusufu akamwangukia babaye usoni, akamlilila, akambusu. Yusufu akawaagiza watumishi wake waganga, kwamba wampake baba yake dawa asioze. Waganga wakampaka dawa Israeli. Siku zake arobaini zikaisha, maana hivyo hutimizwa siku za kupaka dawa. Wamisri wakamlilia siku sabini. Siku za kumlilia zilipopita, Yusufu alisema na watu wa nyumba ya Farao, akinena, Kama nimeona neema machoni penu, tafadhalini mkaseme masikioni mwa Farao, mkinena, Baba yangu aliniapisha, akisema, Mimi ni katika kufa, unizike katika kaburi langu nililojichimbia katika nchi ya Kanaani. Basi tafadhali uniruhusu niende sasa nikamzike babangu, nami nitarudi. Farao akasema, Uende, ukamzike baba yako, kama alivyokuapisha. Basi Yusufu akaenda amzike babaye, na watumwa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, wazee wa nyumbani mwake, na wazee wote wa nchi ya Misri. Na nyumba yote ya Yusufu, na nduguze, na nyumba ya babaye; wakawaacha watoto wao tu, na kondoo zao, na ng’ombe zao, katika nchi ya Gosheni. Kisha wakaenda pamoja naye wapanda farasi, na magari; wakawa jeshi kubwa sana. Wakaja mpaka sakafu ya Atadi, iliyo ng’ambo ya Yordani. Wakaomboleza huko maombolezo makuu, mazito sana. Akafanya matanga ya babaye siku saba. Nao waliokaa katika nchi, wale Wakanaani, walipoyaona matanga katika sakafu ya Atadi, wakasema, Matanga haya ya Wamisri ni makuu kwa hiyo mahali pale paliitwa Abel-Misri, iliyo ng’ambo ya Yordani. Wanawe wakamfanyia kama alivyo waagiza; kwa kuwa wanawe wakamchukuwa mpaka nchi ya Kanaani, nao wakamzika katika pango ya shamba la Makpela, iliyo mbele ya Mamre, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake pa kuzikia.
Mwanzo 50:1-13 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Basi Yusufu akamwangukia baba yake, akalilia juu yake na akambusu. Ndipo Yusufu akawaagiza matabibu waliokuwa wakimhudumia, wamtie baba yake Israeli dawa asioze. Hivyo matabibu wakamtia dawa asioze, wakatumia siku arobaini, muda uliohitajika kutia dawa asioze. Nao Wamisri wakamwombolezea Yakobo kwa siku sabini. Siku za kumwombolezea zilipokwisha, Yusufu akawaambia washauri wa Farao, “Kama nimepata kibali machoni penu semeni na Farao kwa ajili yangu. Mwambieni, ‘Baba yangu aliniapisha na kuniambia, “Mimi niko karibu kufa; unizike katika kaburi lile nililochimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani.” Sasa nakuomba uniruhusu niende kumzika baba yangu, nami nitarudi.’ ” Farao akasema, “Panda, uende kumzika baba yako, kama alivyokuapiza kufanya.” Hivyo Yusufu akapanda kwenda kumzika baba yake. Maafisa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, watu mashuhuri wa baraza lake, na watu mashuhuri wote wa Misri. Hawa ni mbali na watu wote wa nyumbani mwa Yusufu, na ndugu zake, na wale wote wa nyumbani mwa baba yake. Ni watoto wao, makundi yao ya kondoo, mbuzi na ng’ombe tu waliobakia katika nchi ya Gosheni. Magari ya vita na wapanda farasi pia walipanda pamoja naye. Likawa kundi kubwa sana. Walipofika kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Atadi, karibu na Yordani, wakalia kwa sauti na kwa uchungu. Yusufu akakaa huko kwa siku saba kumwombolezea baba yake. Wakanaani walioishi huko walipoona maombolezo yaliyofanyika katika sakafu ile ya kupuria ya Atadi, wakasema, “Wamisri wanafanya maombolezo makubwa.” Kwa hiyo mahali pale karibu na Yordani pakaitwa Abel-Mizraimu. Hivyo wana wa Yakobo wakafanya kama baba yao alivyowaagiza: Wakamchukua hadi nchi ya Kanaani, wakamzika kwenye pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre, ambalo Ibrahimu alilinunua kutoka kwa Efroni Mhiti pamoja na shamba liwe mahali pa kuzikia.