Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 50:1-13

Mwanzo 50:1-13 SRUV

Yusufu akamwangukia babaye usoni, akamlilila, akambusu. Yusufu akawaagiza watumishi wake waganga wampake baba yake dawa asioze. Waganga wakampaka dawa Israeli. Siku zake arubaini zikaisha, maana siku hizo zilitimiza siku za wale waliohifadhiwa kwa kupakwa dawa. Wamisri wakamwombolezea siku sabini. Siku za kumwombolezea zilipopita, Yusufu alisema na watu wa nyumba ya Farao, akinena, Kama nimeona neema machoni penu, tafadhalini mkaseme masikioni mwa Farao, mkinena, Baba yangu aliniapisha, akisema, Mimi ni katika kufa, unizike katika kaburi langu nililojichimbia katika nchi ya Kanaani. Basi tafadhali uniruhusu niende sasa nikamzike babangu, nami nitarudi. Farao akasema, Nenda, ukamzike baba yako, kama alivyokuapisha. Basi Yusufu akaenda kumzika baba yake, na watumishi wote wa Farao wakaenda pamoja naye, wazee wa nyumbani mwake, na wazee wote wa nchi ya Misri. Na nyumba yote ya Yusufu, na ndugu zake, na nyumba ya baba yake; wakawaacha watoto wao tu, na kondoo wao, na ng'ombe wao, katika nchi ya Gosheni. Kisha wakaenda pamoja naye wapanda farasi, na magari; wakawa jeshi kubwa sana. Wakaja mpaka uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, uliyo ng'ambo ya Yordani. Wakaomboleza huko maombolezo makuu, mazito sana. Akafanya matanga ya baba yake siku saba. Nao waliokaa katika nchi, wale Wakanaani, walipoyaona matanga katika sakafu ya Atadi, wakasema, Matanga haya ya Wamisri ni makuu kwa hiyo mahali pale paliitwa Abel-Misri, iliyo ng'ambo ya Yordani. Wanawe wakamfanyia kama alivyowaagiza; kwa kuwa wanawe wakamchukua mpaka nchi ya Kanaani, na wakamzika katika pango ya shamba la Makpela, iliyo mbele ya Mamre, aliyoinunua Abrahamu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia.

Soma Mwanzo 50