Ezra 3
3
Madhabahu yajengwa tena
1Mwezi wa saba ulipowadia baada ya Waisraeli kukaa katika miji yao, watu wote walikusanyika huko Yerusalemu kama mtu mmoja. 2Yeshua mwana wa Yosadaki na makuhani wenzake, Zerubabeli mwana wa Shealtieli pamoja na wenzake walianza kujenga madhabahu ya Mungu wa Israeli ili kumtolea dhabihu za sadaka za kuteketezwa kwa moto, kulingana na ilivyoandikwa katika Torati ya Musa mtu wa Mungu. 3Ingawa waliwaogopa watu waliowazunguka, walijenga madhabahu juu ya ule msingi wake, wakamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu za sadaka za kuteketezwa za asubuhi na za jioni. 4Kisha kulingana na kile kilichoandikwa, wakaiadhimisha Sikukuu ya Vibanda wakitoa idadi ya sadaka za kuteketezwa kama ilivyohitajika kila siku sawasawa na ilivyoagizwa. 5Baada ya hayo, walitoa sadaka za kuteketezwa za kawaida, sadaka za Mwezi Mwandamo na dhabihu zote za sikukuu takatifu za Mwenyezi Mungu zilizoamriwa, pamoja na zile sadaka za hiari zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu. 6Ingawa bado msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu ulikuwa haujawekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba.
Kujenga upya Hekalu
7Kisha watu wakawapa mafundi wa uashi na useremala fedha, wakawapa watu wa Sidoni na Tiro vyakula, vinywaji na mafuta ili waweze kuleta magogo ya mwerezi kupitia bahari kutoka Lebanoni hadi Yafa, kama alivyoagiza Koreshi mfalme wa Uajemi.
8Katika mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kufika kwenye nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki na ndugu zao wengine (makuhani, Walawi na wote waliorejea Yerusalemu kutoka uhamishoni) walianza kazi, wakiteua Walawi wenye umri wa miaka ishirini na zaidi kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu. 9Yeshua na wanawe, pamoja na ndugu zake, Kadmieli na wanawe (wazao wa Hodavia), wana wa Henadadi na wana wao na ndugu zao, Walawi wote walijiunga pamoja kusimamia wale waliofanya kazi katika nyumba ya Mungu.
10Wajenzi walipoweka msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao wakiwa na tarumbeta na Walawi (wana wa Asafu) wakiwa na matoazi, walishika nafasi zao za kumhimidi Mwenyezi Mungu, kama ilivyoagizwa na Daudi mfalme wa Israeli. 11Waliimba nyimbo za sifa na za shukrani kwa Mwenyezi Mungu hivi:
“Yeye ni mwema;
upendo wake kwa Israeli
wadumu milele.”
Watu wote wakapaza sauti kubwa za sifa kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu msingi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu ulikuwa umewekwa. 12Lakini wengi wa makuhani wazee, Walawi na viongozi wa jamaa waliokuwa wameona Hekalu la mwanzoni, walilia kwa sauti walipoona msingi wa Hekalu hili ukiwekwa, huku wengine wengi wakipiga kelele kwa furaha. 13Hakuna mtu ambaye angeweza kutofautisha sauti hizo za furaha na za kilio, kwa sababu watu walipiga kelele sana. Nayo hiyo sauti ikasikika mbali.
Iliyochaguliwa sasa
Ezra 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.