Ezra 4
4
Upinzani kuhusu ujenzi mpya
1Adui za Yuda na Benyamini waliposikia kwamba watu waliorudi kutoka uhamishoni wanajenga Hekalu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, 2wakamjia Zerubabeli na viongozi wa jamaa, nao wakasema, “Turuhusuni tuwasaidie kujenga, kwa sababu sisi tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi na tumekuwa tukimtolea dhabihu tangu wakati wa Esar-Hadoni mfalme wa Ashuru, aliyetuleta hapa.”
3Lakini Zerubabeli, Yeshua na viongozi wengine wa jamaa ya Israeli wakawajibu, “Ninyi hamna sehemu nasi katika kujenga Hekalu la Mungu wetu. Sisi peke yetu tutajenga Hekalu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kama Mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi alivyotuagiza.”
4Ndipo watu waliowazunguka wakajipanga kuwakatisha tamaa watu wa Yuda na kuwafanya waogope walipokuwa wakiendelea na ujenzi. 5Wakaajiri washauri kuwapinga katika kazi yao, nao wakaipinga mipango yao wakati wote wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi hadi wakati wa utawala wa Dario mfalme wa Uajemi.
Upinzani wakati wa wafalme Ahasuero na Artashasta
6Hapo mwanzo wa utawala wa Ahasuero, hao adui waliandika mashtaka dhidi ya watu wa Yuda na Yerusalemu.
7Pia katika siku za utawala wa Artashasta mfalme wa Uajemi, Bishlamu, Mithredathi, Tabeeli pamoja na wenzao waliandika barua kwa Artashasta. Barua hiyo iliandikwa kwa mwandiko wa Kiaramu na katika lugha ya Kiaramu.
8Rehumu afisa msimamizi na mwandishi Shimshai waliandika barua kwa Mfalme Artashasta dhidi ya watu wa Yerusalemu kama ifuatavyo:
9Rehumu afisa msimamizi na mwandishi Shimshai, pamoja na wenzao, yaani mahakimu na maafisa walio juu ya watu kuanzia Tripoli, Uajemi, Ereki na Babeli, Waelami wa Shushani, 10na watu wengine ambao mheshimiwa Asur-Banipali#4:10 yaani Osnapaliau Asnapalikwa Kiaramu. aliwahamisha na kuwakalisha katika mji wa Samaria na mahali pengine Ng’ambo ya Mto Frati.
11(Hii ndiyo nakala ya barua waliyompelekea.)
Kwa Mfalme Artashasta,
Kutoka kwa watumishi wako, watu wa Ng’ambo ya Mto Frati:
12Yapasa Mfalme ajue kuwa Wayahudi waliopanda kuja kwetu kutoka kwenu, wameenda Yerusalemu nao wanaujenga upya ule mji wa uasi na uovu. Wanajenga kuta upya na kukarabati misingi yake.
13Zaidi ya hayo, yampasa mfalme ajue kwamba kama mji huu ukijengwa na kuta zake zikafanywa upya, hakutakuwa na ulipaji wa kodi wala ada au ushuru, hivyo hazina za mfalme zitaathirika. 14Sisi sasa kwa kuwa tunawajibika kwa jumba la kifalme na kwamba siyo sawasawa kwetu kuona mfalme akidharauliwa, basi tunatuma ujumbe huu kumtaarifu mfalme, 15ili ufanyike uchunguzi kwenye kumbukumbu ya maandishi ya waliokutangulia. Katika kumbukumbu hizi utagundua kwamba mji huu ni mwasi, unaowataabisha wafalme na majimbo, ni mahali pa maasi tangu zamani. Ndiyo maana mji huu uliharibiwa. 16Tunamjulisha mfalme kwamba kama mji huu ukijengwa na kuta zake zikifanywa upya, hutabakiwa na chochote Ng’ambo ya Mto Frati.
17Mfalme alirudisha jibu hili:
Kwa Rehumu, afisa msimamizi, mwandishi Shimshai na wenzenu wote wanaoishi katika Samaria na penginepo Ng’ambo ya Mto Frati:
Salamu.
18Barua mliyotutumia imesomwa na kutafsiriwa mbele yangu. 19Nilitoa amri na uchunguzi ukafanyika na imegundulika kwamba mji huu una historia ndefu ya maasi dhidi ya wafalme na pamekuwa mahali pa maasi na uchochezi. 20Yerusalemu umepata kuwa na wafalme wenye nguvu wakitawala nchi yote iliyo Ng’ambo ya Mto Frati, wakitoza kodi, ada na ushuru huko. 21Kwa hiyo toeni amri kwa watu hawa wasimamishe ujenzi, ili mji huu usiendelee kujengwa hadi nitakapoagiza. 22Mwe waangalifu msipuuze jambo hili. Kwa nini kuruhusu tishio hili kuendelea na kusababisha hasara kwa ufalme?
23Mara waliposomewa nakala ya barua ya Mfalme Artashasta, Rehumu na Shimshai aliyekuwa mwandishi na wenzao, walienda mara moja kwa Wayahudi huko Yerusalemu na kuwalazimisha kwa nguvu kusimamisha ujenzi.
24Hivyo kazi ya ujenzi wa nyumba ya Mungu huko Yerusalemu ikasimamishwa kabisa hadi mwaka wa pili wa utawala wa Dario mfalme wa Uajemi.
Iliyochaguliwa sasa
Ezra 4: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.