Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezra 3:8-13

Ezra 3:8-13 NENO

Katika mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kufika kwenye nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki na ndugu zao wengine (makuhani, Walawi na wote waliorejea Yerusalemu kutoka uhamishoni) walianza kazi, wakiteua Walawi wenye umri wa miaka ishirini na zaidi kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu. Yeshua na wanawe, pamoja na ndugu zake, Kadmieli na wanawe (wazao wa Hodavia), wana wa Henadadi na wana wao na ndugu zao, Walawi wote walijiunga pamoja kusimamia wale waliofanya kazi katika nyumba ya Mungu. Wajenzi walipoweka msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao wakiwa na tarumbeta na Walawi (wana wa Asafu) wakiwa na matoazi, walishika nafasi zao za kumhimidi Mwenyezi Mungu, kama ilivyoagizwa na Daudi mfalme wa Israeli. Waliimba nyimbo za sifa na za shukrani kwa Mwenyezi Mungu hivi: “Yeye ni mwema; upendo wake kwa Israeli wadumu milele.” Watu wote wakapaza sauti kubwa za sifa kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu msingi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu ulikuwa umewekwa. Lakini wengi wa makuhani wazee, Walawi na viongozi wa jamaa waliokuwa wameona Hekalu la mwanzoni, walilia kwa sauti walipoona msingi wa Hekalu hili ukiwekwa, huku wengine wengi wakipiga kelele kwa furaha. Hakuna mtu ambaye angeweza kutofautisha sauti hizo za furaha na za kilio, kwa sababu watu walipiga kelele sana. Nayo hiyo sauti ikasikika mbali.