Ezr 3:8-13
Ezr 3:8-13 SUV
Hata mwaka wa pili wa kufika kwao nyumbani kwa Mungu, huko Yerusalemu, mwezi wa pili, Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zao wengine, makuhani na Walawi, na watu wote, waliotoka katika uhamisho na kufika Yerusalemu, wakaanza; nao wakawaweka Walawi, hao wenye miaka ishirini na waliozidi, ili kuisimamia kazi ya nyumba ya BWANA. Ndipo wakasimama Yeshua, na wanawe na ndugu zake, Kadmieli, na wanawe, wana wa Hodavia, pamoja, ili kuwasimamia hao wafanyao kazi katika nyumba ya Mungu; wana wa Henadadi, pamoja na wana wao, na ndugu zao, Walawi. Hata wajenzi walipouweka msingi wa hekalu la BWANA, wakawaweka makuhani, wamevaa mavazi yao, wenye baragumu, na Walawi, wana wa Asafu, wenye matoazi, ili wamhimidi BWANA, kama alivyoagiza Daudi, mfalme wa Israeli. Wakaimbiana, wakimhimidi BWANA, na kumshukuru, wakasema, Kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake kwa Israeli ni za milele. Kisha watu wote wakapaza sauti zao, na kupiga kelele, walipomhimidi BWANA, kwa sababu msingi wa nyumba ya BWANA umekwisha kuwekwa. Bali makuhani wengi, na Walawi, na wakuu wa mbari za mababa, waliokuwa wameiona nyumba ya kwanza, wakati msingi wa nyumba hii ulipowekwa mbele ya macho yao, walilia kwa sauti kuu; na watu wengi walipiga kelele za furaha; hata watu wasiweze kupambanua kelele za furaha, na kelele za vilio vya watu; maana watu walipiga kelele kwa sauti kuu, na kelele zao zikasikilikana mbali sana.