Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 45

45
Mgawanyo wa nchi
1“ ‘Mtakapogawa nchi kuwa urithi, mtaitoa sehemu ya nchi kwa Mwenyezi Mungu kuwa eneo takatifu, urefu wake dhiraa elfu ishirini na tano#45:1 Dhiraa 25,000 ni sawa na kilomita 11.25., na upana wake dhiraa elfu ishirini#45:1 Dhiraa 20,000 ni sawa na kilomita 9.; eneo hili lote litakuwa takatifu. 2Katika eneo hilo patakuwa na sehemu mraba ambayo ni ya mahali patakatifu; kila upande utakuwa dhiraa mia tano, ikiwa imezungukwa na eneo la wazi lenye upana wa dhiraa hamsini. 3Katika eneo takatifu, pima sehemu yenye urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi#45:3 Dhiraa 10,000 ni sawa na kilomita 4.5.. Ndani ya hilo eneo kutakuwa mahali patakatifu, ndipo Patakatifu pa Patakatifu. 4Itakuwa sehemu takatifu ya nchi kwa ajili ya makuhani, wale wanaohudumu ndani ya mahali patakatifu na ambao hukaribia ili kuhudumu mbele za Mwenyezi Mungu. Patakuwa mahali pa nyumba zao pamoja na sehemu kwa ajili ya mahali patakatifu. 5Eneo la urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano, na upana wa dhiraa elfu kumi litakuwa la Walawi, wanaohudumu hekaluni, kama milki yao kwa ajili ya miji ya kuishi.
6“ ‘Utatoa mji kama mali yao, wenye upana wa dhiraa elfu tano#45:6 Dhiraa 5,000 ni sawa na kilomita 2.25., na urefu wa dhiraa elfu ishirini na tano karibu na sehemu takatifu; itakuwa mali ya nyumba yote ya Israeli.
7“ ‘Mkuu anayetawala atakuwa na eneo linalopakana na lile eneo lililowekwa wakfu kwa upande moja, na eneo la mji upande mwingine. Eneo la mji litaenea upande wa magharibi kuanzia upande wa magharibi, na kuenea mashariki kuanzia upande wa mashariki, likiendelea kwa urefu kutoka magharibi hadi mpaka wa mashariki, sambamba na mojawapo ya sehemu za makabila. 8Nchi hii itakuwa milki yake katika Israeli. Nao wakuu wangu hawatawadhulumu tena watu wangu, bali watairuhusu nyumba ya Israeli kuimiliki nchi kulingana na makabila yao.
9“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Yatosha, enyi wakuu wa Israeli! Acheni mbali ukatili wenu na uonevu wenu mkafanye lile lililo haki na sawa. Acheni kuwatoza watu wangu isivyo haki, asema Bwana Mungu Mwenyezi. 10Tumieni mizani sahihi na vipimo sahihi vya efa#45:10 Efa ni kipimo cha ujazo cha kupimia vitu vikavu ambacho ni sawa na omeri 10; efa 1 ni sawa na kilo 22. na bathi#45:10 Bathi ni kipimo cha ujazo cha kupimia vitu vya humiminika ambacho ni sawa na 1/10 ya homeri; homeri 1 ni bathi 10 au efa 10.. 11Efa na bathi viwe sawa, bathi iwe sehemu ya kumi ya homeri na efa iwe sehemu ya kumi ya homeri, homeri itakuwa ndicho kiwango cha kukubalika kwa vyote viwili. 12Shekeli moja itakuwa gera ishirini. Shekeli ishirini, jumlisha na shekeli ishirini na tano, jumlisha na shekeli kumi na tano zitakuwa mina moja#45:12 Mina 1 hapa ni sawa na shekeli 60; mina ya kawaida ilikuwa sawa na shekeli 50..
Sadaka na siku takatifu
(Kutoka 12:1-20; Walawi 23:33-43)
13“ ‘Hili ndilo toleo maalum mtakalotoa: sehemu ya sita ya efa kutoka kila homeri ya ngano, na sehemu ya sita ya efa kutoka kila homeri ya shayiri. 14Sehemu ya mafuta iliyoamriwa, yaliyopimwa kwa bathi, ni sehemu ya kumi ya bathi kutoka kila kori moja (ambayo ina bathi kumi au homeri moja, kwa kuwa bathi kumi ni homeri moja). 15Pia kondoo mmoja atachukuliwa kutoka kila kundi la kondoo mia mbili katika malisho yenye maji mengi ya Israeli. Hivi vitatumika kwa ajili ya sadaka ya nafaka, sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani ili kufanya upatanisho kwa ajili ya watu, asema Bwana Mungu Mwenyezi. 16Watu wote wa nchi wataungana pamoja katika kutoa sadaka hii maalum ya kutumiwa na mkuu anayetawala Israeli. 17Utakuwa wajibu wa mkuu anayetawala kutoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji kwenye sikukuu, Mwezi Mwandamo na Sabato, kwenye sikukuu zote zilizoamriwa za nyumba ya Israeli. Atatoa sadaka za dhambi, sadaka za nafaka, sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ya Israeli.
18“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya huo mwezi utamchukua fahali mchanga asiye na dosari na kutakasa mahali patakatifu. 19Kuhani itampasa achukue sehemu ya hiyo damu ya sadaka ya dhambi na kuipaka kwenye miimo ya Hekalu, kwenye pembe nne za juu za ukingo wa hayo madhabahu na juu ya miimo ya lango la ukumbi wa ndani. 20Itakupasa kufanya vivyo hivyo katika siku ya saba ya mwezi huo kwa ajili ya mtu ambaye hutenda dhambi bila kukusudia au bila kujua; ndivyo utafanya upatanisho kwa ajili ya Hekalu.
21“ ‘Katika mwezi wa kwanza siku ya kumi na nne utaadhimisha Pasaka. Sikukuu itaendelea kwa siku saba, wakati huo wa hizo siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. 22Katika siku hiyo mkuu anayetawala atatoa fahali kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote wa nchi. 23Kila siku wakati wa hizo siku saba za sikukuu atatoa mafahali saba na kondoo dume saba wasio na dosari kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu na beberu kwa ajili ya sadaka ya dhambi. 24Pia atatoa sadaka ya nafaka efa moja kwa kila fahali, na efa moja kwa kila kondoo dume, pamoja na hini moja#45:24 Hini ni kipimo cha kupimia vitu vya humiminika chenye ujazo wa 1/6 ya bathi, na ni sawa na lita 4. ya mafuta kwa kila efa.
25“ ‘Wakati wa hizo siku saba za sikukuu, ambayo huanza katika mwezi wa saba kwenye siku ya kumi na tano, mkuu anayetawala atatoa mahitaji yale yale kwa ajili ya sadaka za dhambi, sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta.

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 45: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia