Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 44

44
Mkuu, Walawi, makuhani
1Ndipo yule mtu akanirudisha mpaka kwenye lango la nje la mahali patakatifu, lile linaloelekea upande wa mashariki, nalo lilikuwa limefungwa. 2Mwenyezi Mungu akaniambia, “Lango hili litabaki limefungwa. Haliruhusiwi kufunguliwa, wala hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingilia kwenye lango hili. Litabaki limefungwa kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ameingia kupitia lango hili. 3Yeye aliye mkuu peke yake ndiye anayeweza kukaa penye njia ya hilo lango na kula chakula mbele za Mwenyezi Mungu. Itampasa aingie kwa njia hiyo ya lango la ukumbini na kutokea njia hiyo hiyo.”
4Kisha yule mtu akanileta kwa njia ya lango la kaskazini mpaka mbele ya Hekalu. Nikatazama nami nikauona utukufu wa Mwenyezi Mungu ukilijaza Hekalu la Mwenyezi Mungu, nami nikaanguka kifudifudi.
5Mwenyezi Mungu akaniambia, “Mwanadamu, angalia kwa uangalifu, usikilize kwa makini na uzingatie kila kitu ninachokuambia kuhusu masharti yote yanayohusu Hekalu la Mwenyezi Mungu. Uwe mwangalifu kuhusu wale wanaoruhusiwa hekaluni na wale wasioruhusiwa kuingia mahali patakatifu. 6Iambie nyumba ya uasi ya Israeli, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Matendo yenu ya machukizo yatosha, ee nyumba ya Israeli! 7Zaidi ya matendo yenu yote ya machukizo, mmewaleta wageni wasiotahiriwa mioyo na miili katika patakatifu pangu. Mmelinajisi Hekalu langu, huku mkinitolea chakula, mafuta ya wanyama na damu, nanyi mmevunja agano langu. 8Badala ya kutimiza wajibu wenu kuhusiana na vitu vyangu vitakatifu, mmeweka watu wengine kuwa viongozi katika patakatifu pangu. 9Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Hakuna mgeni asiyetahiriwa moyo na mwilini anayeruhusiwa kuingia patakatifu pangu, wala hata wageni wanaoishi miongoni mwa Waisraeli.
10“ ‘Walawi walioniacha wakati Waisraeli walipopotoka wakatoka kwangu na kutangatanga kwa kufuata sanamu zao, sharti watachukua adhabu ya dhambi zao. 11Wanaweza wakatumika katika mahali patakatifu pangu, wakiwa na uangalizi wa malango ya Hekalu; wanaweza kuchinja wanyama wa sadaka za kuteketezwa, na kutoa dhabihu kwa ajili ya watu, na kusimama mbele ya watu ili kuwahudumia. 12Lakini kwa sababu walitumikia watu wakiwa mbele ya sanamu zao, na kuifanya nyumba ya Israeli ianguke kwenye dhambi, kwa hiyo nimeapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba ni lazima wachukue matokeo ya dhambi yao, asema Bwana Mungu Mwenyezi. 13Hawaruhusiwi kukaribia ili kunitumikia kama makuhani wala kukaribia chochote changu kilicho kitakatifu au sadaka iliyo takatifu kupita zote, bali watachukua aibu ya matendo yao ya kuchukiza. 14Lakini nitawaweka katika uangalizi wa Hekalu na kazi zote zile zinazotakiwa kufanyika ndani yake.
15“ ‘Lakini makuhani, ambao ni Walawi na wazao wa Sadoki, ambao walitimiza wajibu wao kwa uaminifu katika patakatifu pangu wakati Waisraeli walipopotoka, watakaribia ili kutumika mbele zangu. Itawapasa wasimame mbele zangu ili kutoa dhabihu za mafuta ya wanyama na damu, asema Bwana Mungu Mwenyezi. 16Wao peke yao ndio wenye ruhusa ya kuingia mahali patakatifu pangu. Wao peke yao ndio watakaokaribia meza yangu ili kuhudumu mbele zangu na kufanya utumishi wangu.
17“ ‘Watakapoingia kwenye malango ya ukumbi wa ndani, watavaa nguo za kitani safi, hawaruhusiwi kamwe kuvaa mavazi ya sufu wakati wanapokuwa wakihudumu kwenye malango ya ukumbi wa ndani wala ndani ya Hekalu. 18Watavaa vilemba vya kitani safi vichwani mwao na nguo za ndani za kitani safi viunoni mwao. Hawatavaa chochote kitakachowafanya kutoa jasho. 19Watakapotoka ili kuingia katika ukumbi wa nje mahali watu walipo, watavua nguo walizokuwa wakihudumu nazo na wataziacha katika vyumba vitakatifu nao watavaa nguo nyingine, ili wasije wakaambukiza watu utakatifu kupitia mavazi yao.
20“ ‘Hawatanyoa nywele za vichwa vyao wala kuziacha ziwe ndefu, bali watazipunguza. 21Kuhani yeyote asinywe mvinyo aingiapo katika ukumbi wa ndani. 22Wasioe wanawake wajane wala walioachika, inawapasa kuoa wanawake bikira wenye heshima wa Israeli au wajane wa makuhani. 23Watawafundisha watu wangu tofauti kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida na kuwaonesha jinsi ya kupambanua kati ya vitu najisi na vitu safi.
24“ ‘Katika magombano yoyote, makuhani watatumika kama mahakimu na kuamua hilo jambo kufuatana na sheria zangu. Watazishika sheria zangu na maagizo yangu katika sikukuu zangu zote zilizoamriwa, nao watatakasa Sabato zangu.
25“ ‘Kuhani asijitie unajisi kwa kukaribia maiti; lakini, ikiwa mtu aliyekufa alikuwa baba yake au mama yake, mwana au binti yake, ndugu yake au dada ambaye hakuolewa, basi anaweza kujitia unajisi kwa hao. 26Baada ya kujitakasa, atakaa hali hiyo kwa muda wa siku saba. 27Siku atakapoingia katika ukumbi wa ndani wa mahali patakatifu ili kuhudumu, atatoa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
28“ ‘Mimi ndio nitakuwa urithi pekee wa makuhani katika Israeli. Msiwape wao milki, mimi nitakuwa milki yao. 29Wao watakula sadaka za nafaka, sadaka za dhambi na sadaka za hatia na kila kitu kitakachotolewa kwa Mwenyezi Mungu katika Israeli kitakuwa chao. 30Yote yaliyo bora ya malimbuko ya vitu vyote na matoleo yenu maalum vitakuwa vya makuhani. Inawapasa kuwapa malimbuko ya kwanza ya unga wenu ili baraka ipate kuwa katika nyumba zenu. 31Makuhani hawaruhusiwi kula chochote, ikiwa ni ndege au mnyama, aliyekutwa amekufa au aliyeraruliwa na wanyama pori.

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 44: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia