Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 46

46
Sheria nyingine mbalimbali
1“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Lango la ukumbi wa ndani linaloelekea upande wa mashariki litakuwa linafungwa kwa siku sita za juma, ila siku ya Sabato na siku ya Mwezi Mwandamo litafunguliwa. 2Mkuu anayetawala ataingia kupitia baraza ya njia ya lango la ukumbi na kusimama karibu na nguzo ya lango. Makuhani watatoa sadaka za mkuu anayetawala za kuteketezwa na sadaka za amani. Mkuu anayetawala atasujudu kwenye kizingiti cha njia ya lango, kisha atatoka nje, lakini lango halitafungwa hadi jioni. 3Siku za Sabato na za Mwezi Mwandamo watu wote wa nchi wataabudu mbele za Mwenyezi Mungu penye lile ingilio la ile njia. 4Sadaka za kuteketezwa aletazo mkuu anayetawala kwa Mwenyezi Mungu siku ya Sabato zitakuwa ni wana-kondoo sita na kondoo dume mmoja, wote wasiwe na dosari. 5Sadaka ya nafaka inayotolewa pamoja na huyo kondoo dume itakuwa efa moja, na sadaka ya nafaka inayotolewa na hao wana-kondoo itakuwa kiasi apendacho mtu pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa. 6Siku ya Mwezi Mwandamo atatoa fahali mchanga, wana-kondoo sita na kondoo dume, wote wasiwe na dosari. 7Atatoa sadaka ya nafaka ya: efa moja kwa huyo fahali, na efa moja kwa huyo kondoo dume; na kwa wana-kondoo atatoa nafaka nyingi kama atakavyo kutoa; atatoa hini ya mafuta kwa kila efa. 8Mkuu anayetawala atakapoingia, atapitia kwenye baraza ya njia ya lango, naye atatoka nje kwa njia hiyo hiyo.
9“ ‘Watu wa nchi wanapokuja mbele za Mwenyezi Mungu katika sikukuu zilizoamriwa, yeyote aingiaye kwa lango la kaskazini kuabudu atatoka nje kwa lango la kusini; na yeyote aingiaye kwa lango la kusini atatoka nje kwa lango la kaskazini. Hakuna mtu yeyote atakayerudi kupitia lango lile aliloingilia, lakini kila mmoja atatoka nje kwa lango linalokabili lile aliloingilia. 10Mkuu anayetawala atakuwa miongoni mwao, akiingia nao ndani wanapoingia, na akitoka nao nje wanapotoka.
11“ ‘Kwenye sikukuu na kwenye sikukuu zilizoamriwa, sadaka ya nafaka itakuwa efa moja pamoja na fahali mmoja, efa moja pamoja na kondoo dume mmoja, pamoja na idadi ya wana-kondoo kama mtu apendavyo kutoa, pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa. 12Mkuu anayetawala anapotoa sadaka ya hiari kwa Mwenyezi Mungu, iwe ni sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya amani, atafunguliwa lango linaloelekea mashariki. Atatoa sadaka yake ya kuteketezwa au sadaka yake ya amani kama afanyavyo katika siku ya Sabato. Kisha atatoka nje. Baada yake kutoka nje, lango litafungwa.
13“ ‘Kila siku utamtoa mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiyekuwa na dosari kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi Mungu, utaitoa kila siku asubuhi. 14Pia kila siku asubuhi pamoja na hiyo sadaka utatoa sadaka ya nafaka, ikiwa na sehemu ya sita ya efa#46:14 Sehemu ya sita ya efa ni sawa na kilo 2.7. pamoja na theluthi moja ya hini#46:14 Theluthi moja ya hini ni sawa na lita 1.3. ya mafuta ya kuchanganya na ule unga. Utoaji wa sadaka hii ya nafaka kwa Mwenyezi Mungu ni agizo la kudumu. 15Kwa hiyo mwana-kondoo na sadaka ya nafaka na mafuta vitatolewa kila siku asubuhi kwa ajili ya sadaka ya daima ya kuteketezwa.
16“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ikiwa mkuu anayetawala atatoa zawadi kutoka urithi wake na kumpa mmoja wa wanawe, hiyo zawadi itakuwa pia kwa wazao wake; itakuwa mali yao kwa urithi. 17Hata hivyo, kama atatoa zawadi kutoka urithi wake na kumpa mmoja wa watumishi wake, mtumishi anaweza kuiweka hadi mwaka wa uhuru, kisha itarudishwa kwa mkuu anayetawala. Urithi wake ni wa wanawe peke yao, ni mali yao. 18Mkuu anayetawala hafai kuchukua urithi wowote wa watu na kuwaondoa kwenye mali yao. Mkuu huyo atawapa wanawe urithi wao katika mali yake mwenyewe, ili pasiwe na mtu wangu yeyote atakayetengwa na urithi wake.’ ”
19Kisha mtu yule akanileta kupitia kwenye ingilio lililokuwa kando ya lango hadi kwenye vyumba vitakatifu vilivyoelekea kaskazini, ambavyo ni vya makuhani, naye akanionesha mahali fulani upande wa mwisho wa magharibi. 20Akaniambia, “Mahali hapa ndipo makuhani watakapotokosea sadaka ya hatia na sadaka ya dhambi, na kuoka sadaka ya nafaka, ili kuepuka kuzileta katika ukumbi wa nje na kushirikisha utakatifu kwa watu.”
21Baada ya hapo akanileta kwenye ukumbi wa nje na kunizungusha kwenye pembe zake nne, nami nikaona katika kila pembe ya huo ukumbi kulikuwa na ukumbi mwingine. 22Katika pembe nne za huo ukumbi wa nje kulikuwa na kumbi nyingine, zenye urefu wa dhiraa arobaini na upana wake dhiraa thelathini, ambapo hizo kumbi kwenye hizo pembe nne zilikuwa na vipimo vilivyo sawa. 23Mzunguko wa ndani wa hizo kumbi nne ulikuwa na ukingo wa jiwe, zikiwa na sehemu zilizojengwa kwa ajili ya moto kuzunguka chini ya huo ukingo. 24Akaniambia, “Hizi ndizo sehemu za kupikia ambazo wale wanaohudumu kwenye Hekalu watatokosea dhabihu za watu.”

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 46: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia