Ezekieli 28:1-10
Ezekieli 28:1-10 NENO
Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, mwambie mfalme wa Tiro, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Kwa sababu moyo wako umejivuna na umesema, “Mimi ni mungu; nami ninaketi kwenye kiti cha enzi cha mungu katika moyo wa bahari.” Lakini wewe ni mwanadamu, wala si mungu, ingawa unafikiri kuwa una hekima kama mungu. Je, wewe una hekima kuliko Danieli? Je, hakuna siri iliyofichika kwako? Kwa hekima yako na ufahamu wako, umejipatia utajiri, nawe umejikusanyia dhahabu na fedha katika hazina zako. Kwa werevu wako mwingi katika biashara, umeongeza utajiri wako na kwa sababu ya utajiri wako moyo wako umekuwa na kiburi. “ ‘Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: “ ‘Kwa sababu unafikiri una hekima, mwenye hekima kama mungu, mimi nitawaleta wageni dhidi yako, taifa katili kuliko yote; watafuta panga zao dhidi ya uzuri wa hekima yako, na kuchafua fahari yako inayong’aa. Watakushusha chini shimoni, nawe utakufa kifo cha kikatili katika moyo wa bahari. Je, wakati huo utasema, “Mimi ni mungu,” mbele ya wale wanaokuua? Utakuwa mwanadamu tu, wala si mungu, mikononi mwa hao wanaokuua. Utakufa kifo cha wasiotahiriwa kwa mkono wa wageni. Kwa kuwa mimi nimenena, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”