Ezekieli 28:1-10
Ezekieli 28:1-10 SRUV
Neno la BWANA likanijia tena, kusema, Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu. Tazama, una hekima kuliko Danieli; hapana neno la siri watu wawezalo kukuficha; kwa hekima yako na kwa fahamu zako umejipatia utajiri, nawe umepata dhahabu na fedha katika hazina zako; kwa hekima yako nyingi, na kwa biashara yako, umeongeza utajiri wako, na moyo wako umeinuka kwa sababu ya utajiri wako; basi, kwa hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu; basi, tazama, nitaleta wageni juu yako, watu wa mataifa wenye kutisha; nao watafuta panga zao juu ya uzuri wa hekima yako, nao watautia uchafu mwangaza wako. Watakushusha hadi shimoni; nawe utakufa kifo chao waliouawa kati ya bahari. Je! Utazidi kusema mbele yake huyo akuuaye, Mimi ni mungu? Lakini u mwanadamu, wala si Mungu, mkononi mwake akutiaye jeraha. Utakufa kifo cha hao wasiotahiriwa, kwa mikono ya wageni; kwa maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU.