Ezekieli 28:1-10
Ezekieli 28:1-10 BHN
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Mwambie mfalme wa Tiro kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wewe una kiburi cha moyo, na umesema kwamba wewe ni mungu, kwamba umekalia kiti cha enzi cha miungu, umekaa mbali huko baharini. Lakini, wewe ni binadamu tu wala si Mungu, ingawa wajiona kuwa una hekima kama Mungu. Haya! Wewe wajiona mwenye hekima kuliko Danieli, wadhani hakuna siri yoyote usiyoijua. Kwa hekima na akili yako umejipatia utajiri, umejikusanyia dhahabu na fedha ukaziweka katika hazina zako. Kwa busara yako kubwa katika biashara umejiongezea utajiri wako, ukawa na kiburi kwa mali zako! Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa vile unajiona mwenye hekima kama Mungu, basi nitakuletea watu wageni, mataifa katili kuliko yote. Wataharibu fahari ya hekima yako na kuchafua uzuri wako. Watakutumbukiza chini shimoni, nawe utakufa kifo cha kikatili kilindini mwa bahari. Je, utajiona bado kuwa mungu mbele ya hao watakaokuua? Mikononi mwa hao watakaokuangamiza, utatambua kuwa wewe ni mtu tu, wala si Mungu! Utakufa kifo cha aibu kubwa mikononi mwa watu wa mataifa. Ni mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”