Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 28

28
Unabii dhidi ya mfalme wa Tiro
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, mwambie mfalme wa Tiro, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“ ‘Kwa sababu moyo wako umejivuna
na umesema, “Mimi ni mungu;
nami ninaketi kwenye kiti cha enzi cha mungu
katika moyo wa bahari.”
Lakini wewe ni mwanadamu, wala si mungu,
ingawa unafikiri kuwa una hekima kama mungu.
3Je, wewe una hekima kuliko Danieli?
Je, hakuna siri iliyofichika kwako?
4Kwa hekima yako na ufahamu wako,
umejipatia utajiri,
nawe umejikusanyia dhahabu
na fedha katika hazina zako.
5Kwa werevu wako mwingi katika biashara,
umeongeza utajiri wako
na kwa sababu ya utajiri wako
moyo wako umekuwa na kiburi.
6“ ‘Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“ ‘Kwa sababu unafikiri una hekima,
mwenye hekima kama mungu,
7mimi nitawaleta wageni dhidi yako,
taifa katili kuliko yote;
watafuta panga zao dhidi ya uzuri wa hekima yako,
na kuchafua fahari yako inayong’aa.
8Watakushusha chini shimoni,
nawe utakufa kifo cha kikatili
katika moyo wa bahari.
9Je, wakati huo utasema, “Mimi ni mungu,”
mbele ya wale wanaokuua?
Utakuwa mwanadamu tu, wala si mungu,
mikononi mwa hao wanaokuua.
10Utakufa kifo cha wasiotahiriwa
kwa mkono wa wageni.
Kwa kuwa mimi nimenena, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
11Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 12“Mwanadamu, mfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, nawe umwambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“ ‘Ulikuwa kipeo cha ukamilifu, ukiwa umejaa hekima
na mkamilifu katika uzuri.
13Ulikuwa ndani ya Edeni,
bustani ya Mungu;
kila kito cha thamani kilikupamba:
akiki nyekundu, yakuti manjano na zumaridi,
krisolitho, shohamu na yaspi,
yakuti samawi, almasi na zabarajadi.
Kuwekwa kwa hayo mapambo na kushikizwa kwake
kulifanywa kwa dhahabu;
siku ile ulipoumbwa yaliandaliwa tayari.
14Ulipakwa mafuta kuwa kerubi mlinzi,
kwa kuwa hivyo ndivyo nilivyokuweka wakfu.
Ulikuwa kwenye mlima mtakatifu wa Mungu;
ulitembea katikati ya vito vya moto.
15Ulikuwa mnyofu katika njia zako
tangu siku ile ya kuumbwa kwako,
hadi uovu ulipoonekana ndani yako.
16Kutokana na biashara yako iliyoenea,
ulijazwa na dhuluma,
nawe ukatenda dhambi.
Hivyo nilikuondoa kwa aibu kutoka mlima wa Mungu,
nami nikakufukuza, ee kerubi mlinzi,
kutoka katikati ya vito vya moto.
17Moyo wako ukawa na kiburi
kwa ajili ya uzuri wako,
nawe ukaiharibu hekima yako
kwa sababu ya fahari yako.
Kwa hiyo nikakutupa chini;
nimekufanya kioja mbele ya wafalme.
18Kwa dhambi zako nyingi na biashara yako ya dhuluma,
umenajisi mahali pako patakatifu.
Kwa hiyo nilifanya moto utoke ndani yako,
nao ukakuteketeza,
nami nikakufanya majivu juu ya nchi,
machoni pa wote waliokuwa wakitazama.
19Mataifa yote yaliyokujua
yanakustaajabia;
umefikia mwisho wa kutisha
na hutakuwepo tena milele.’ ”
Unabii dhidi ya Sidoni
20Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 21“Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Sidoni, ukatabiri dhidi yake, 22nawe useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“ ‘Mimi ni kinyume chako, ee Sidoni,
nami nitapata utukufu ndani yako.
Nao watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu,
nitakapotekeleza hukumu zangu
na kuonesha utakatifu wangu ndani yake.
23Nitapeleka tauni ndani yake
na kufanya damu itiririke katika barabara zake.
Waliochinjwa wataanguka ndani yake,
kwa upanga dhidi yake kila upande.
Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
24“ ‘Nyumba ya Israeli hawatakuwa tena na majirani wenye nia ya kuwadhuru, wanaoumiza kama michongoma na miiba mikali. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi.
25“ ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitakapoikusanya nyumba ya Israeli kutoka mataifa ambako wametawanyika, nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwao machoni pa mataifa. Ndipo watakapoishi katika nchi yao wenyewe, niliyompa mtumishi wangu Yakobo. 26Wataishi humo kwa salama na watajenga nyumba na kupanda mashamba ya mizabibu, wataishi kwa salama nitakapowaadhibu majirani zao wote ambao waliwafanyia uovu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wao.’ ”

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 28: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia