Ezekieli 25
25
Unabii dhidi ya Amoni
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Waamoni utabiri dhidi yao. 3Waambie, ‘Sikieni neno la Bwana Mungu Mwenyezi. Hili ndilo Bwana Mungu Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ulisema, “Aha!” juu ya mahali pangu patakatifu palipotiwa unajisi, na juu ya nchi ya Israeli ilipoangamizwa, na juu ya watu wa Yuda walipoenda uhamishoni, 4kwa hiyo nitawatia mikononi mwa watu wa mashariki mkawe mali yao. Watapiga kambi zao kati yenu na kufanya makazi miongoni mwenu, watakula matunda yenu na kunywa maziwa yenu. 5Nitaufanya mji wa Raba kuwa malisho ya ngamia na Amoni kuwa mahali pa kondoo pa kupumzikia. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu. 6Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa kuwa mmepiga makofi yenu na kufanya kishindo kwa miguu, mkifurahia kwa mioyo yenu miovu juu ya yale mabaya yaliyoipata nchi ya Israeli, 7hivyo nitaunyoosha mkono wangu dhidi yenu na kuwatoa kuwa nyara kwa mataifa. Nitawakatilia mbali kutoka mataifa na kuwang’oa kutoka nchi. Nitawaangamiza, nanyi mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
Unabii dhidi ya Moabu
8“Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: ‘Kwa sababu Moabu na Seiri wamesema, “Tazama, nyumba ya Yuda imekuwa kama mataifa mengine yote,” 9kwa hiyo nitaiondoa ile miji iliyo kando ya Moabu, kuanzia miji iliyo mipakani: Beth-Yeshimothi, Baal-Meoni na Kiriathaimu, iliyo utukufu wa nchi hiyo. 10Nitaitia Moabu pamoja na Waamoni mikononi mwa watu wa Mashariki kuwa milki yao, ili Waamoni wasikumbukwe miongoni mwa mataifa, 11nami nitatoa adhabu kwa Moabu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”
Unabii dhidi ya Edomu
12“Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: ‘Kwa sababu Edomu walilipiza kisasi juu ya nyumba ya Yuda, wakakosea sana kwa kufanya hivyo, 13kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitaunyoosha mkono wangu dhidi ya Edomu na kuua watu wake na wanyama wao. Nitaufanya ukiwa, na kuanzia Temani hadi Dedani wataanguka kwa upanga. 14Nitalipiza Edomu kisasi kwa mkono wa watu wangu Israeli, nao watawatendea Edomu sawasawa na hasira yangu na ghadhabu yangu, nao watakijua kisasi changu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
Unabii dhidi ya Ufilisti
15“Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: ‘Kwa sababu Wafilisti wamewalipiza kisasi kwa uovu wa mioyo yao na kwa uadui wa siku nyingi wakataka kuangamiza Yuda, 16kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi ninakaribia kuunyoosha mkono wangu dhidi ya Wafilisti, nami nitawakatilia mbali Wakerethi na kuwaangamiza wale waliosalia katika pwani. 17Nitalipiza kisasi kikubwa juu yao na kuwaadhibu katika ghadhabu yangu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapolipiza kisasi juu yao.’ ”
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 25: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.