Ezekieli 26
26
Unabii dhidi ya Tiro
1Mwaka wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, kwa sababu Tiro amesema kuhusu Yerusalemu, ‘Aha! Lango la kwenda kwa mataifa limevunjika, nayo milango yake iko wazi mbele yangu, sasa kwa kuwa amekuwa magofu nitastawi.’ 3Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi niko kinyume na wewe, ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi dhidi yako, kama bahari inayovurumisha mawimbi yake. 4Watavunja kuta za Tiro na kuibomoa minara yake, nitakwangua udongo wake na kuufanya mwamba mtupu. 5Itakuwa huko katikati ya bahari patakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki, kwa maana nimenena, asema Bwana Mungu Mwenyezi. Atakuwa nyara kwa mataifa, 6nayo makazi yake huko bara yataangamizwa kwa upanga. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
7“Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kutoka kaskazini nitamleta dhidi ya Tiro Mfalme Nebukadneza wa Babeli, mfalme wa wafalme, akiwa na farasi na magari ya vita, wapanda farasi na jeshi kubwa. 8Atayaharibu makazi yako huko bara kwa upanga; atajenga husuru dhidi yako, na kupandisha kilima hadi kuta zako, na kuinua ngao zake dhidi yako. 9Ataelekeza mapigo ya magogo ya kubomoa boma dhidi ya kuta zako, na kubomoa minara yako kwa silaha zake. 10Farasi wake watakuwa wengi sana kiasi kwamba utafunikwa na mavumbi watakayotimua. Kuta zako zitatikisika kwa mshindo wa farasi wa vita, magari ya kukokotwa, na magari ya vita wakati aingiapo malango yako kama watu wanaoingia mji ambao kuta zake zimebomolewa kote.
11“Kwato za farasi wake zitakanyaga barabara zako zote, atawaua watu wako kwa upanga na nguzo zako zilizo imara zitaanguka chini. 12Watateka utajiri wako na kuchukua nyara bidhaa zako, watazivunja kuta zako na kuzibomoa nyumba zako nzuri, watatupa baharini mawe yako, mbao zako na kifusi chako. 13Nitakomesha kelele za nyimbo zako, na uimbaji wako wa kinubi kamwe hautasikika tena. 14Nitakufanya mwamba mtupu, nawe utakuwa mahali pa kutandazia nyavu za kuvulia samaki. Kamwe hutajengwa tena, kwa maana Mimi Mwenyezi Mungu nimenena, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
15“Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa Tiro: ‘Je, nchi za pwani hazitatetemeka kwa kishindo cha anguko lako, wakati majeruhi wanapolia kwa maumivu makali na wakati mauaji yanaendelea ndani yako? 16Ndipo wakuu wote wa mataifa ya pwani watashuka kutoka viti vyao vya utawala, na kuweka kando majoho yao na kuvua nguo zao zilizotariziwa. Wataketi chini ardhini, wakiwa wamevikwa hofu kuu, wakitetemeka kila dakika na kukustaajabia. 17Ndipo wao watakuombolezea na kukuambia:
“ ‘Tazama jinsi ulivyoharibiwa,
ee mji uliokuwa na sifa,
wewe uliyekaliwa na mabaharia!
Ulikuwa na nguvu kwenye bahari,
wewe na wakaaji wako;
wote walioishi huko,
uliwatia hofu kuu.
18Sasa nchi za pwani zinatetemeka
katika siku ya anguko lako;
visiwa vilivyomo baharini
vinaogopa kwa kuporomoka kwako.’
19“Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitakapokufanya uwe mji wa ukiwa, kama miji isiyokaliwa tena na watu, nitakapoleta vilindi vya bahari juu yako na maji yake makuu yatakapokufunika, 20ndipo nitakapokushusha chini pamoja na wale wanaoshuka shimoni, kwa watu wa kale, nami nitakufanya uishi katika pande za chini za nchi kama katika magofu ya kale, pamoja na wale wanaoshuka shimoni, nawe hutarudi au kurejea kwenye makao yako katika nchi ya walio hai. 21Nitakufikisha mwisho wa kutisha wala hutakuwepo tena. Watu watakutafuta, lakini kamwe hutaonekana tena, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”
Iliyochaguliwa sasa
Ezekieli 26: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.