Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 24

24
Chungu cha kupikia
1Katika mwaka wa tisa, mwezi wa kumi, siku ya kumi, neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, weka kumbukumbu ya tarehe hii, tarehe hii hasa, kwa kuwa mfalme wa Babeli ameuzingira mji wa Yerusalemu kwa jeshi siku hii ya leo. 3Nenea nyumba hii ya uasi kwa fumbo, uwaambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“ ‘Teleka sufuria jikoni; iteleke
na umimine maji ndani yake,
4Weka vipande vya nyama ndani yake,
vipande vyote vizuri, vya paja na vya bega.
Ijaze hiyo sufuria kwa mifupa hii mizuri;
5chagua yule aliye bora wa kundi la kondoo.
Panga kuni chini ya sufuria kwa ajili ya mifupa;
chochea hadi ichemke
na uitokose hiyo mifupa ndani yake.
6“ ‘Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“ ‘Ole wa mji unaomwaga damu,
ole wa sufuria ambayo sasa ina ukoko ndani yake,
ambayo ukoko wake hautoki.
Kipakue kipande baada ya kipande,
bila kuvipigia kura.
7“ ‘Kwa kuwa damu aliyoimwaga ipo katikati yake:
Huyo mwanamke aliimwaga juu ya mwamba ulio wazi;
hakuimwaga kwenye ardhi,
ambako vumbi lingeifunika.
8Kuchochea ghadhabu na kulipiza kisasi,
nimemwaga damu yake
juu ya mwamba ulio wazi,
ili isifunikwe.
9“ ‘Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“ ‘Ole wa mji unaomwaga damu!
Mimi nami nitalundikia kuni nyingi.
10Kwa hiyo lundika kuni
na uwashe moto.
Pika hiyo nyama vizuri,
changanya vikolezo ndani yake,
na uiache mifupa iungue kwenye moto.
11Kisha teleka sufuria tupu kwenye makaa
hadi iwe na moto sana na shaba yake ing’ae,
ili uchafu wake upate kuyeyuka
na ukoko wake upate kuungua na kuondoka.
12Imezuia juhudi zote,
ukoko wake mwingi haujaondoka,
hata ikiwa ni kwa moto.
13“ ‘Sasa uchafu wako ni uasherati wako. Kwa sababu nilijaribu kukutakasa lakini haikuwezekana kutakaswa kutokana na huo uchafu wako, hutatakasika tena hadi ghadhabu yangu dhidi yako iwe imepungua.
14“ ‘Mimi Mwenyezi Mungu nimesema, wakati umewadia wa mimi kutenda. Mimi sitazuia, mimi sitaona huruma wala sitapunguza hasira yangu. Utahukumiwa sawasawa na mwenendo na matendo yako, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
Kifo cha mke wa Ezekieli
15Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 16“Mwanadamu, kwa pigo moja nakaribia kukuondolea kile kilicho furaha ya macho yako. Lakini usiomboleze au kulia wala kudondosha machozi yoyote. 17Lia kwa uchungu kimya kimya usimwombolezee mtu aliyekufa. Jifunge kilemba chako na uvae viatu vyako miguuni mwako, usifunike sehemu ya chini ya uso wako, wala usile vyakula vya waombolezaji.”
18Hivyo nikanena na watu asubuhi na jioni mke wangu akafa. Kesho yake asubuhi nilifanya kama nilivyoamriwa.
19Ndipo watu wakaniuliza, “Je, jambo hili unalofanya linamaanisha nini kwetu?”
20Kwa hiyo nikawaambia, “Neno la Mwenyezi Mungu lilinijia kusema: 21‘Sema na nyumba ya Israeli. Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninakaribia kupatia unajisi mahali pangu patakatifu, ngome ambayo ndani yake mnaona fahari, furaha ya macho yenu, kitu mnachokipenda. Wana wenu wa kiume na wa kike mliowaacha nyuma wataanguka kwa upanga. 22Nanyi mtafanya kama nilivyofanya. Hamtafunika sehemu ya chini ya nyuso zenu wala hamtakula vyakula vya kawaida vya waombolezaji. 23Mtajifunga vilemba vichwani mwenu na kuvaa viatu vyenu miguuni mwenu. Hamtaomboleza au kulia, lakini mtadhoofika kwa sababu ya dhambi zenu na kulia kwa uchungu kila mtu na mwenzake. 24Ezekieli atakuwa ishara kwenu, mtafanya kama yeye alivyofanya. Jambo hili litakapotokea, mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi.’
25“Nawe, mwanadamu, siku ile nitakapoondoa ngome yao iliyo furaha yao na utukufu wao, kitu cha kupendeza macho yao, kile kilicho shauku ya mioyo yao, wana wao wa kiume na wa kike vilevile, 26siku hiyo atakayetoroka atakuja kuwapasha habari. 27Katika siku ile kinywa chako kitamfumbukia yeye aliyenusurika, nawe utaongea wala hutanyamaza tena. Hivyo wewe utakuwa ishara kwao, nao watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 24: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia