Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 23

23
Dada wawili makahaba
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2“Mwanadamu, palikuwa na wanawake wawili, binti za mama mmoja. 3Wakawa makahaba huko Misri, wakajitia kwenye ukahaba tangu ujana wao. Katika nchi ile vifua vyao vya ubikira vikakumbatiwa, na wakapoteza ubikira wao. 4Mkubwa aliitwa Ohola, na mdogo wake Oholiba. Walikuwa wangu nao wakazaa watoto wa kiume na wa kike. Ohola ni Samaria, Oholiba ni Yerusalemu.
5“Ohola akajitia kwenye ukahaba alipokuwa bado ni wangu, akatamani sana wapenzi wake, mashujaa Waashuru, 6waliovaa nguo za buluu, watawala na majemadari, wote walikuwa wanaume vijana wa kuvutia, wapandao farasi. 7Akafanya ukahaba na wakuu wote wa Ashuru, na kujinajisi kwa sanamu zote za kila mwanaume aliyemtamani. 8Hakuacha ukahaba wake aliouanza huko Misri, wakati wa ujana wake ambapo wanaume walilala naye, wakikumbatia kifua cha ubikira wake na kumwaga tamaa zao juu yake.
9“Kwa hiyo nilimtia mikononi mwa wapenzi wake, Waashuru, kwa kuwa ndio aliowatamani. 10Wakamvua nguo zake wakamwacha uchi, wakawachukua wanawe wa kiume na wa kike, naye wakamuua kwa upanga. Akawa kitu cha kudharauliwa miongoni mwa wanawake, na adhabu ikatolewa dhidi yake.
11“Oholiba dada yake aliliona jambo hili, lakini kwa tamaa zake na ukahaba wake, akaharibu tabia zake kuliko Ohola, dada yake. 12Yeye naye aliwatamani Waashuru, watawala na majemadari, mashujaa waliovalia sare, wapandao farasi, wanaume vijana wote waliovutia. 13Nikaona kuwa yeye pia alijinajisi, wote wawili wakaelekea njia moja.
14“Lakini yeye akazidisha ukahaba wake. Akaona wanaume waliochorwa ukutani, picha za Wakaldayo#23:14 yaani Wababeli waliovalia nguo nyekundu, 15wakiwa na mikanda viunoni mwao na vilemba vichwani mwao, wote walifanana na maafisa wa Babeli wapandao magari ya vita, wenyeji wa Ukaldayo#23:15 yaani Babeli. 16Mara tu alipowaona, aliwatamani, akatuma wajumbe kwao huko Ukaldayo. 17Ndipo hao Wababeli wakaja kwake kwenye kitanda cha mapenzi, nao katika tamaa zao wakamtia unajisi. Baada ya kutiwa unajisi, akawaacha kwa kuwachukia. 18Alipofanya ukahaba wake waziwazi na kuonesha uchi wake, nilimwacha kwa kumchukia, kama vile nilivyokuwa nimemwacha dada yake. 19Lakini akazidisha ukahaba wake alipozikumbuka siku za ujana wake, alipokuwa kahaba huko Misri. 20Huko aliwatamani wapenzi wake, ambao viungo vyao vya uzazi ni kama vya punda, na kile kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi. 21Hivyo ulitamani uasherati wa ujana wako wakati ulipokuwa Misri, kifua chako kilipokumbatiwa, na matiti yako machanga yakapapaswa.
22“Kwa hiyo, Oholiba, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitawachochea wapenzi wako wawe kinyume na wewe, wale uliowaacha kwa kuchukia, nitawaleta dhidi yako kutoka kila upande: 23Wababeli na Wakaldayo wote, watu kutoka Pekodi, na Shoa na Koa, wakiwa pamoja na Waashuru wote, vijana wazuri, wote wakiwa watawala na majemadari, maafisa wa magari ya vita na watu wa vyeo vya juu, wote wakiwa wamepanda farasi. 24Watakuja dhidi yako wakiwa na silaha, magari ya vita, magari ya kukokota, pamoja na umati mkubwa wa watu. Watakuzingira pande zote kwa ngao na vigao na kwa chapeo. Nitakutia mikononi mwao ili wakuadhibu, nao watakuadhibu sawasawa na sheria zao. 25Nitaelekeza hasira yangu yenye wivu dhidi yako, nao watakuadhibu kwa hasira kali. Watakatilia mbali pua yako na masikio yako, na wale watakaosalia miongoni mwako watauawa kwa upanga. Watachukua wana wako wa kiume na wa kike, na wale watakaosalia miongoni mwenu watateketezwa kwa moto. 26Watakuvua nguo zako pia, na kuchukua mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito na dhahabu. 27Hivyo ndivyo nitakavyokomesha uasherati wako na ukahaba wako uliouanza huko Misri. Hutatazama vitu hivi kwa kuvitamani wala kukumbuka Misri tena.
28“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninakaribia kukutia mikononi mwa wale unaowachukia, kwa wale uliojitenga nao kwa kuwachukia. 29Watakutenda mambo ya chuki na kukunyang’anya kila kitu ulichokifanyia kazi. Watakuacha uchi na mtupu na aibu ya ukahaba wako itafunuliwa. Uasherati wako na uzinzi wako 30umekuletea haya yote, kwa sababu ulitamani mataifa na kujinajisi kwa sanamu zao. 31Umeiendea njia ya dada yako, hivyo nitakitia kikombe chake mkononi mwako.
32“Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“Utakinywea kikombe cha dada yako,
kikombe kikubwa na chenye kina kirefu;
kitakuletea dharau na dhihaka,
kwa kuwa kimejaa sana.
33Utalewa ulevi na kujawa huzuni,
kikombe cha maangamizi na ukiwa,
kikombe cha dada yako Samaria.
34Utakinywa chote na kukimaliza;
utakivunja vipande vipande
na kuyararua matiti yako.
Nimenena haya, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
35“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa kuwa ulinisahau mimi na kunitupa nyuma yako, lazima ubebe matokeo ya uasherati wako na ukahaba wako.”
36Mwenyezi Mungu akaniambia, “Mwanadamu, je, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi wakabili kwa ajili ya matendo yao ya machukizo, 37kwa kuwa wamefanya uzinzi na damu imo mikononi mwao. Wamefanya uzinzi na sanamu zao, hata watoto walionizalia wamewatoa kafara, kuwa chakula kwa sanamu hizo. 38Pia wamenifanyia hili: wakati huo huo wamenajisi patakatifu pangu na kuzitangua Sabato zangu. 39Siku ile ile walitoa kafara watoto wao kwa sanamu zao, waliingia patakatifu pangu na kupanajisi. Hilo ndilo walilolifanya katika nyumba yangu.
40“Hata waliwatuma wajumbe kuwaita watu kutoka mbali, nao walipowasili ulioga kwa ajili yao, ukapaka macho yako wanja, na ukavaa mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito vya dhahabu. 41Ukaketi kwenye kiti cha anasa, kukiwa na meza iliyoandaliwa mbele yake ambayo juu yake ulikuwa umeweka uvumba na mafuta ambayo yalikuwa yangu.
42“Kelele za umati wa watu wasiojali zilikuwa zimemzunguka, wakaleta watu wengi waliokuwa wakifanya makelele na walevi kutoka nyikani, ambao walitia bangili kwenye mikono ya yule mwanamke na dada yake na pia taji nzuri za kupendeza kwenye vichwa vyao. 43Ndipo nikasema kuhusu yule aliyechakazwa na uzinzi, ‘Basi wamtumie kama kahaba, kwa kuwa ndivyo alivyo.’ 44Nao wakazini naye. Kama vile watu wazinivyo na kahaba, ndiyo hivyo walivyozini na hao wanawake waasherati, Ohola na Oholiba. 45Lakini watu wenye haki, watawahukumia adhabu wanawake wafanyao uzinzi na kumwaga damu, kwa kuwa ni wazinzi na damu iko mikononi mwao.
46“Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Leteni watu wengi wenye makelele dhidi yao na uwaache wapate hofu na watekwe nyara. 47Hao watu wengi watawapiga kwa mawe na kuwaua kwa panga zao, watawaua wana wao wa kiume na wa kike, na kuzichoma nyumba zao.
48“Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi, ili wanawake wote wapate onyo nao wasije wakafanya uasherati kama ninyi mlivyofanya. 49Utapata adhabu kwa ajili ya uasherati wako na kuchukua matokeo ya dhambi zako za uasherati. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi.”

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 23: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia