Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 18:1-12

Kutoka 18:1-12 NENO

Basi Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Musa, akawa amesikia kila kitu Mungu alichomfanyia Musa na watu wake wa Israeli, pia jinsi Mwenyezi Mungu alivyowatoa Israeli Misri. Baada ya Musa kumrudisha mkewe Sipora, Yethro baba mkwe wake alimpokea pamoja na wanawe wawili. Jina la mmoja aliitwa Gershomu, kwa kuwa Musa alisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.” Mwingine aliitwa Eliezeri, kwa kuwa alisema, “Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa kutoka upanga wa Farao.” Yethro, baba mkwe wa Musa, pamoja na wana wawili wa Musa na mkewe, wakamjia Musa huko jangwani, mahali alipokuwa amepiga kambi karibu na mlima wa Mungu. Yethro alikuwa ametuma ujumbe kwake Musa, kusema, “Mimi Yethro baba mkwe wako ninakuja kwako pamoja na mke wako na wanao wawili.” Kwa hiyo Musa akatoka kumlaki baba mkwe wake, akainama na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia kwenye hema. Musa akamwambia baba mkwe wake kuhusu kila kitu Mwenyezi Mungu alichomfanyia Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na pia kuhusu shida zote walizokutana nazo njiani, na jinsi Mwenyezi Mungu alivyowaokoa. Yethro akafurahishwa sana kusikia kuhusu mambo yote mazuri Mwenyezi Mungu aliyowatendea Waisraeli kuwaokoa kutoka mkono wa Wamisri. Yethro akasema, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, aliyekuokoa wewe kutoka mikononi mwa Wamisri na Farao, na aliyewaokoa watu kutoka mikononi mwa Wamisri. Sasa najua ya kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu kuliko miungu mingine yote, kwa kuwa amewatendea hivi wale waliowatenda Israeli kwa ujeuri.” Kisha Yethro, baba mkwe wa Musa, akaleta sadaka ya kuteketezwa na dhabihu nyingine kwa Mungu, naye Haruni pamoja na wazee wote wa Israeli wakaja kula chakula pamoja na baba mkwe wa Musa mbele za Mungu.

Video ya Kutoka 18:1-12