Kutoka 18
18
Yethro amtembelea Musa
1Basi Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Musa, akawa amesikia kila kitu Mungu alichomfanyia Musa na watu wake wa Israeli, pia jinsi Mwenyezi Mungu alivyowatoa Israeli Misri.
2Baada ya Musa kumrudisha mkewe Sipora, Yethro baba mkwe wake alimpokea 3pamoja na wanawe wawili. Jina la mmoja aliitwa Gershomu, kwa kuwa Musa alisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.” 4Mwingine aliitwa Eliezeri, kwa kuwa alisema, “Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa kutoka upanga wa Farao.”
5Yethro, baba mkwe wa Musa, pamoja na wana wawili wa Musa na mkewe, wakamjia Musa huko jangwani, mahali alipokuwa amepiga kambi karibu na mlima wa Mungu. 6Yethro alikuwa ametuma ujumbe kwake Musa, kusema, “Mimi Yethro baba mkwe wako ninakuja kwako pamoja na mke wako na wanao wawili.”
7Kwa hiyo Musa akatoka kumlaki baba mkwe wake, akainama na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia kwenye hema. 8Musa akamwambia baba mkwe wake kuhusu kila kitu Mwenyezi Mungu alichomfanyia Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na pia kuhusu shida zote walizokutana nazo njiani, na jinsi Mwenyezi Mungu alivyowaokoa.
9Yethro akafurahishwa sana kusikia kuhusu mambo yote mazuri Mwenyezi Mungu aliyowatendea Waisraeli kuwaokoa kutoka mkono wa Wamisri. 10Yethro akasema, “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, aliyekuokoa wewe kutoka mikononi mwa Wamisri na Farao, na aliyewaokoa watu kutoka mikononi mwa Wamisri. 11Sasa najua ya kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu kuliko miungu mingine yote, kwa kuwa amewatendea hivi wale waliowatenda Israeli kwa ujeuri.” 12Kisha Yethro, baba mkwe wa Musa, akaleta sadaka ya kuteketezwa na dhabihu nyingine kwa Mungu, naye Haruni pamoja na wazee wote wa Israeli wakaja kula chakula pamoja na baba mkwe wa Musa mbele za Mungu.
Ushauri wa Yethro
(Kumbukumbu 1:9-18)
13Siku iliyofuata, Musa akachukua nafasi yake kama hakimu wa watu, nao wakasimama kumzunguka kuanzia asubuhi hadi jioni. 14Baba mkwe wake alipoona yote Musa anayowafanyia watu, akasema, “Ni nini hiki unachowafanyia watu? Kwa nini wewe unakuwa mwamuzi wa watu hawa peke yako, wakati watu hawa wamesimama wakikuzunguka tangu asubuhi hadi jioni?”
15Musa akamjibu, “Kwa sababu watu wananijia kutaka mapenzi ya Mungu. 16Kila wakiwa na shauri huletwa kwangu, nami huamua kati ya mtu na mwenzake, na kuwaeleza hukumu na sheria zake Mungu.”
17Baba mkwe wa Musa akamjibu, “Unachofanya sio kizuri. 18Wewe pamoja na watu hawa wanaokujia mtajichosha bure. Kazi ni nzito sana kwako, huwezi kuibeba mwenyewe. 19Sasa nisikilize mimi, nitakupa ushauri, naye Mungu na awe pamoja nawe. Yapasa wewe uwe mwakilishi wa watu mbele za Mungu na ulete mashauri yao kwake. 20Wafundishe hukumu na sheria zake, na uwaoneshe jinsi wanavyopaswa kuishi, na jinsi wanavyopaswa kuenenda. 21Lakini uchague watu wenye uwezo miongoni mwa watu wote, watu wanaomwogopa Mungu, watu waaminifu wanaochukia mali ya dhuluma, uwateuwe wawe maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. 22Waweke wawe waamuzi wa watu kwa wakati wote, lakini waambie wakuletee kila shauri lililo gumu; yale yaliyo rahisi wayaamue wao wenyewe. Hii itafanya mzigo wako kuwa mwepesi, kwa sababu watashirikiana nawe. 23Ukifanya hivi, na ikiwa Mungu ameagiza hivyo, utaweza kushinda uchovu, nao watu hawa wote watarudi nyumbani wameridhika.”
Kuchaguliwa kwa waamuzi
24Musa akamsikiliza baba mkwe wake na kufanya kila kitu alichosema. 25Musa akawachagua watu wenye uwezo kutoka Israeli yote, akawafanya wawe viongozi wa watu, maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. 26Wakatumika kama waamuzi wa watu kwa wakati wote. Mashauri magumu wakayaleta kwa Musa, lakini yale yaliyo rahisi wakayaamua wenyewe.
27Kisha Musa akaagana na Yethro baba mkwe wake, naye akarudi kwa nchi yake.
Iliyochaguliwa sasa
Kutoka 18: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.