Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 18:1-12

Kutoka 18:1-12 SRUV

Basi Yethro, kuhani wa Midiani, mkwewe Musa, alisikia habari ya mambo hayo yote Mungu aliyokuwa amemtendea Musa, na Waisraeli watu wake, jinsi BWANA alivyowaleta Israeli watoke Misri. Ndipo Yethro mkwewe Musa akamtwaa Sipora, mke wa Musa, baada ya yeye kumrudisha, pamoja na wanawe wawili; katika hao, jina la mmoja ni Gershomu, maana alisema, Mimi nimekuwa mgeni katika nchi za kigeni; na jina la wa pili ni Eliezeri, kwa kuwa alisema, Yeye Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa na upanga wa Farao. Basi Yethro, mkwewe Musa, pamoja na mke wa Musa na wanawe wawili wakamwendea Musa huko nyikani, hapo alipokuwa amepiga kambi, kwenye mlima wa Mungu; naye akamwambia Musa, Mimi Yethro mkweo nimekuja kwako, na mkeo, na wanawe wawili pamoja naye. Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe, akasujudia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani. Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote BWANA aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote yaliyowapata njiani, na jinsi BWANA alivyowaokoa. Yethro alifurahi kwa ajili ya wema wote BWANA aliowatendea Israeli, kwa alivyowaokoa mikononi mwa Wamisri. Kisha Yethro akasema, Na ahimidiwe BWANA aliyewaokoa na mikono ya Wamisri, na mkono wa Farao; aliyewaokoa watu hao watoke mikononi mwa Wamisri. Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa ujeuri. Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu.

Soma Kutoka 18

Video ya Kutoka 18:1-12