Esta 2
2
Esta afanywa malkia
1Baadaye, wakati hasira ya Mfalme Ahasuero ilikuwa imetulia, alimkumbuka Vashti na kile alichokuwa amekifanya, na alilokuwa ameamuru juu yake. 2Kisha watumishi waliomhudumia mfalme walipendekeza, “Watafutwe wanawali mabikira wazuri wa sura kwa ajili ya mfalme. 3Mfalme na awateue maafisa katika kila jimbo la himaya yake kuwaleta hao wanawali wote wazuri wa sura katika nyumba ya wanawake katika ngome ya mji wa Shushani. Kisha wawekwe chini ya uangalizi wa Hegai, towashi wa mfalme, aliyekuwa msimamizi wa wanawake; na wapewe huduma zote za urembo. 4Kisha yule ambaye atampendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti.” Shauri hili likampendeza mfalme, naye akalifuata.
5Basi katika mji wa ngome ya Shushani palikuwa na Myahudi wa kabila la Benyamini, jina lake Mordekai mwana wa Yairi, mwana wa Shimei, mwana wa Kishi, 6ambao walichukuliwa uhamishoni kutoka Yerusalemu na Mfalme Nebukadneza wa Babeli, wakiwa miongoni mwa waliochukuliwa mateka pamoja na Mfalme Yekonia wa Yuda. 7Mordekai alikuwa na binamu yake msichana aliyeitwa Hadasa, ambaye alimlea kwa kuwa hakuwa na baba wala mama. Msichana huyu, ambaye pia alijulikana kwa jina la Esta, alikuwa na umbo na sura ya kupendeza, naye Mordekai alimtunza kama binti yake mwenyewe baada ya baba yake na mama yake kufariki.
8Agizo na amri ya mfalme ilipotangazwa, wanawali wengi waliletwa kwenye ngome ya mji wa Shushani na kuwekwa chini ya uangalizi wa Hegai. Pia Esta alipelekwa katika jumba la mfalme na akakabidhiwa kwa Hegai, aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake. 9Msichana huyu alimpendeza na kupata kibali mbele zake. Mara moja akaanza kumpa matunzo ya urembo na chakula maalum. Alimpa Esta vijakazi saba waliochaguliwa kutoka jumba la kifalme, na kumhamishia yeye pamoja na vijakazi wake katika sehemu bora zaidi katika nyumba ya wanawake.
10Esta alikuwa hajadhihirisha uraia wake na asili yake, kwa sababu Mordekai alikuwa amemkataza kufanya hivyo. 11Kila siku Mordekai alikuwa akitembeatembea karibu na ua wa nyumba ya wanawake kujua Esta alivyoendelea na kuona yaliyokuwa yakitendeka kwake.
12Kabla zamu ya msichana haijafika ya kwenda kwa Mfalme Ahasuero, ilimbidi atimize miezi kumi na mbili ya matunzo ya urembo kama ilivyokuwa imepangwa. Kwa miezi sita walikuwa wajipake mafuta ya manemane, na miezi sita kujipaka manukato na vipodozi. 13Basi hivi ndivyo ambavyo msichana angeingia kwa mfalme: Kila kitu alichohitaji aliruhusiwa kuchukua kutoka nyumba ya wanawake na kwenda navyo katika jumba la mfalme. 14Jioni angeenda pale na asubuhi kurudi sehemu nyingine ya nyumba ya wanawake katika utunzaji wa Shaashgazi, towashi wa mfalme aliyekuwa mkuu wa masuria. Hangeweza kurudi kwa mfalme hadi apendezwe naye na kuagiza aitwe kwa jina lake.
15Zamu ya Esta ilipofika kwenda kwa mfalme (msichana ambaye Mordekai alikuwa amemlea, binti Abihaili, mjomba wake), Esta hakutaka vitu zaidi ya vile Hegai, towashi wa mfalme aliyekuwa mkuu wa nyumba ya wanawake, alikuwa amemshauri. Naye Esta alipata kibali kwa kila mtu aliyemwona. 16Esta alipelekwa kwa Mfalme Ahasuero katika makao ya mfalme mwezi wa kumi, yaani mwezi wa Tebethi, katika mwaka wake wa saba wa kutawala.
17Basi mfalme alivutiwa na Esta kuliko wanawake wengine wote, naye akapata upendeleo na kibali kuliko mabikira wengine. Kisha akamvika taji la kifalme kichwani mwake na kumfanya malkia badala ya Vashti. 18Mfalme akafanya karamu kubwa, karamu ya Esta, kwa wakuu wake wote na maafisa. Mfalme akatangaza siku ya mapumziko katika majimbo yake yote na kugawa zawadi kwa ukarimu wa kifalme.
Mordekai agundua hila
19Wakati mabikira walikusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa ameketi katika lango la mfalme. 20Lakini Esta alikuwa ameficha siri ya asili yake na uraia wake, kama Mordekai alivyokuwa amemwambia, kwa maana aliendelea kufuata maelekezo ya Mordekai kama alivyokuwa akifanya alipokuwa akimlea.
21Ikawa Mordekai alipokuwa ameketi kwenye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, maafisa wawili wa mfalme waliokuwa walinzi wa lango, walikasirika na kupanga njama ya kumuua Mfalme Ahasuero. 22Lakini Mordekai aligundua hila hii na kumwambia Malkia Esta, ambaye baadaye alimwarifu mfalme, huku akimsifu Mordekai. 23Taarifa hiyo ilipochunguzwa na kuonekana kuwa kweli, maafisa hao wawili waliangikwa juu ya miti ya kunyongea. Haya yote yaliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.
Iliyochaguliwa sasa
Esta 2: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.