Esta 3
3
Hila ya Hamani kuwaangamiza Wayahudi
1Baada ya matukio haya, Mfalme Ahasuero alimheshimu Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, akampandisha na kumpa kiti chake cha heshima cha juu sana kuliko wakuu wengine wote. 2Maafisa wote wa mfalme waliokaa langoni mwa mfalme walipiga magoti na kumpa Hamani heshima, kwa kuwa mfalme alikuwa ameamuru hili kuhusu Hamani. Lakini Mordekai hakumpigia magoti wala kumheshimu.
3Kisha maafisa wa mfalme waliokuwa langoni mwa mfalme walimuuliza Mordekai, “Kwa nini hutii agizo la mfalme?” 4Siku baada ya siku walizungumza naye lakini hakukubali. Kwa hiyo walimweleza Hamani kuona kama tabia ya Mordekai itaweza kuvumiliwa, kwa maana alikuwa amewaambia kuwa yeye ni Myahudi.
5Hamani alipoona kuwa Mordekai hampigii magoti wala kumpa heshima, alighadhibika. 6Hata hivyo, baada ya kujulishwa watu wa Mordekai ni akina nani, alibadili wazo la kumuua Mordekai peke yake. Badala yake Hamani alitafuta njia ya kuwaangamiza watu wote wa Mordekai, yaani Wayahudi, walio katika ufalme wote wa Ahasuero.
7Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Mfalme Ahasuero, katika mwezi wa kwanza uitwao Nisani, walipiga puri (yaani kura) mbele ya Hamani ili kuchagua siku na mwezi. Kura ikaangukia kwenye mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari.
8Kisha Hamani akamwambia Mfalme Ahasuero, “Wako watu fulani wameenea na kutawanyika miongoni mwa watu katika majimbo yote ya ufalme wako, ambao desturi zao ni tofauti na zile za watu wengine wote, nao hawatii sheria za mfalme. Haifai mfalme kuwavumilia watu hawa. 9Kama inampendeza mfalme, itolewe amri kuwaangamiza, nami nitaweka talanta elfu kumi#3:9 Talanta 10,000 ni sawa na tani 340. za fedha katika hazina ya mfalme kwa ajili ya watu watakaoshughulikia jambo hili.”
10Basi mfalme alichukua pete yake ya muhuri kutoka kidole chake na kumpa Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, adui wa Wayahudi. 11Mfalme akamwambia Hamani, “Baki na fedha yako na uwatendee hao watu utakavyo.”
12Kisha siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza waandishi wa mfalme waliitwa. Wakaandika barua kwa kila jimbo na katika kila lugha ya watu kama agizo la Hamani lilivyotoka kwa mfalme, kwa watawala wa majimbo mbalimbali, na wakuu wa watu mbalimbali. Hizi ziliandikwa kwa jina la Mfalme Ahasuero mwenyewe na kutiwa muhuri wa pete yake mwenyewe. 13Barua zilipelekwa na tarishi katika majimbo yote ya mfalme zikiwa na amri ya kuharibu, kuua na kuangamiza Wayahudi wote, wadogo kwa wakubwa, wanawake na watoto wadogo, siku moja, yaani siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, na pia kuteka nyara vitu vyao. 14Nakala ya andiko la amri ilipaswa kutolewa kama sheria katika kila jimbo, na kufahamishwa kwa watu wa kila taifa ili waweze kuwa tayari kwa siku ile.
15Kwa kuharakishwa na amri ya mfalme, matarishi walienda na andiko lilitolewa katika mji wa ngome ya Shushani. Mfalme na Hamani waliketi na kunywa, lakini mji wa Shushani ulifadhaika.
Iliyochaguliwa sasa
Esta 3: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.