Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 23

23
Kutengwa na mkutano
1Asiingie mtu yeyote aliyehasiwa kwa kupondwa makende au kwa kukatwa uume wake katika kusanyiko la Mwenyezi Mungu.
2Mtu ambaye amezaliwa kwenye ndoa isiyo halali au wazao wake wasiingie kwenye kusanyiko la Mwenyezi Mungu, hata kizazi cha kumi.
3Hapatakuwa na Mwamoni au Mmoabu au yeyote wa wazao wao atakayeruhusiwa kuingia katika kusanyiko la Mwenyezi Mungu, hata kizazi cha kumi. 4Kwa kuwa hawakuja kuwalaki wakiwa na mkate na maji mlipokuwa njiani mkitoka Misri; tena walimwajiri Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia ili awalaani. 5Hata hivyo, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hakumsikiliza Balaamu bali aligeuza laana kuwa baraka kwenu kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapenda. 6Msitafute mapatano ya urafiki nao maisha yenu yote.
7Usimchukie Mwedomu, kwa kuwa yeye ni ndugu yako. Usimchukie Mmisri, kwa sababu uliishi kama mgeni katika nchi yake. 8Kizazi cha tatu cha watoto watakaozaliwa nao wanaweza kuingia katika kusanyiko la Mwenyezi Mungu.
Unajisi katika kambi
9Unapokuwa umepiga kambi dhidi ya adui zako, jitenge na kitu chochote kisicho safi. 10Ikiwa mtu amechafuka kwa sababu ya kutokwa na shahawa usiku, inampasa atoke nje ya kambi na kukaa huko. 11Lakini jioni ikikaribia ataoga, na baada ya jua kuzama ataingia tena kambini.
12Tengeni mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda kujisaidia. 13Kama sehemu ya vifaa vyenu kuweni na kitu cha kulimia, nanyi mnapojisaidia, chimba shimo na kisha funika kinyesi chako. 14Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hutembea katika kambi yenu ili kuwalinda na kuwaweka adui zenu mikononi mwenu. Kambi yenu ni lazima iwe takatifu, ili asione kitu chochote miongoni mwenu kilicho kichafu, akageuka na kuwaacha.
Sheria mbalimbali
15Ikiwa mtumwa amekimbilia kwako, usimrudishe kwa bwana wake. 16Mwache aishi miongoni mwenu mahali popote anapopapenda na katika mji wowote anaochagua. Usimdhulumu.
17Asiwepo Mwisraeli mwanamke kahaba au mwanaume hanithi wa mahali pa ibada za sanamu. 18Kamwe usilete mapato ya ukahaba ikiwa ni ya mwanamke au ni ya mwanaume katika nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yoyote, kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anachukizwa na yote mawili.
19Usimtoze ndugu yako riba, iwe ni fedha ama chakula ama kitu kingine chochote ambacho unaweza kupata riba juu yake. 20Unaweza kumtoza mgeni riba, lakini siyo nduguyo Mwisraeli, ili Mwenyezi Mungu, Mungu wako, akubariki katika kila kitu unachoweka mkono katika nchi unayoingia kuimiliki.
21Ukiweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, usichelewe kuitimiza, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakudai, nawe utakuwa na hatia ya dhambi. 22Lakini ukijizuia kuweka nadhiri, hutakuwa na hatia. 23Chochote kitakachotamkwa kwa midomo yako ni lazima uhakikishe umekifanya, kwa sababu uliweka nadhiri yako kwa hiari mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa kinywa chako mwenyewe.
24Ukiingia katika shamba la mizabibu la jirani yako, unaweza kula zabibu kadiri utakavyo, lakini usiweke chochote kwenye kikapu chako. 25Ukiingia katika shamba la nafaka la jirani yako, unaweza kukwanyua kwa mikono yako, lakini usikate kwa mundu nafaka iliyosimama.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 23: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia