Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 22

22
1Ukimwona ng’ombe au kondoo wa ndugu yako anapotea, usipuuze, bali uhakikishe unamrudisha kwa mwenyewe. 2Ikiwa huyo ndugu haishi karibu nawe au kama wewe hufahamu yeye ni nani, mchukue nyumbani kwako huyo mnyama, umweke hadi mwenyewe aje kumtafuta. Nawe umrudishie. 3Fanya vivyo hivyo ukimkuta punda wa nduguyo au joho lake au chochote alichopoteza. Usipuuze jambo hilo.
4Ukimwona punda wa nduguyo au ng’ombe wake ameanguka barabarani, usipuuze jambo hilo. Msaidie asimame kwa miguu yake.
5Haimpasi mwanamke kuvaa mavazi ya kiume wala mwanaume kuvaa mavazi ya kike, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anachukia yeyote anayefanya hivi.
6Ukikuta kiota cha ndege kando ya barabara, iwe juu ya mti au chini, naye ndege amelala juu ya makinda au mayai, usimchukue huyo ndege pamoja na makinda yake. 7Unaweza kuchukua makinda, lakini hakikisha unamwachilia huyo ndege, ili upate kufanikiwa na kuishi maisha marefu.
8Unapojenga nyumba mpya, fanya ukuta wa kuzuia kandokando ya dari ili usijiletee hatia ya kumwaga damu juu ya nyumba yako ikiwa yeyote ataanguka kutoka humo.
9Usipande aina mbili za mbegu katika shamba lako la mizabibu; ikiwa utafanya hivyo, si mazao utakayopanda tu yatakuwa najisi, bali nayo matunda ya shamba la mizabibu pia.
10Usilime kwa maksai aliyefungwa nira pamoja na punda.
11Usivae nguo za sufu na kitani zilizofumwa pamoja.
12Fanya vishada kwenye pembe nne za joho unalovaa.
Kukiuka taratibu za ndoa
13Ikiwa mtu atamwoa mke na baada ya kufanya naye tendo la ndoa, akamchukia, 14akimsingizia na kumwita jina baya, akisema, “Nilimwoa mwanamke huyu, lakini nilipomkaribia sikupata uthibitisho wa ubikira wake” 15ndipo baba na mama wa msichana wataleta uthibitisho kwamba alikuwa bikira kwa wazee wa mji kwenye lango. 16Baba wa msichana atawaambia wazee, “Nilimwoza binti yangu kwa huyu mwanaume, lakini hampendi. 17Sasa amemsingizia na kusema, ‘Sikumkuta huyu binti akiwa bikira.’ Lakini hapa kuna uthibitisho wa ubikira wa binti yangu.” Kisha wazazi wake wataonesha nguo zake kwa wazee wa mji, 18nao wazee watamchukua huyo mwanaume na kumwadhibu. 19Watamtoza shekeli mia moja#22:19 Shekeli 100 za fedha ni sawa na kilo moja. za fedha na kupewa wazazi wa msichana, kwa sababu mwanaume huyu amempa bikira Mwisraeli jina baya. Ataendelea kuwa mke wake; kamwe hawezi kumpa talaka siku zote za maisha yake.
20Hata hivyo, kama shtaka ni la kweli na hakuna uthibitisho kuhusu ubikira wa huyo msichana uliopatikana, 21huyo msichana ataletwa kwenye mlango wa nyumba ya baba yake, na hapo wanaume wa mji wake watampiga kwa mawe hadi afe. Amefanya kitu cha aibu katika Israeli kwa kufanya ukahaba akiwa nyumbani mwa babaye. Lazima mwondoe uovu kati yenu.
22Ikiwa mwanaume atakutwa akizini na mke wa mtu mwingine, wote wawili, mwanaume na mwanamke aliyezini naye, lazima wauawe. Lazima mwondoe uovu katika Israeli.
23Ikiwa mwanaume atakutana na bikira mjini ambaye ameposwa na mtu akazini naye, 24utawachukua wote wawili kwenye lango la mji na kuwapiga kwa mawe hadi wafe; yule msichana kwa kuwa alikuwa mjini na hakupiga yowe kuomba msaada, na yule mwanaume kwa sababu amemtenda jeuri mke wa mtu mwingine. Lazima mwondoe uovu kati yenu.
25Lakini ikiwa itatokea mwanaume akakutana na msichana aliyeposwa huko mashambani, akambaka, mwanaume aliyefanya hivi peke yake ndiye atakayeuawa. 26Usimtendee msichana yule jambo lolote; hajafanya dhambi inayostahili kifo. Shauri hili ni kama lile la yeyote ambaye anamshambulia na kumuua kwa makusudi jirani yake, 27kwa maana mwanaume huyo alimkuta msichana huko mashambani, na ingawa msichana aliyeposwa alipiga yowe, hapakuwa na mtu wa kumwokoa.
28Ikiwa itatokea mwanaume akutane na bikira ambaye hajaposwa na kumbaka nao wakakutwa, 29mwanaume atamlipa baba wa msichana shekeli hamsini#22:29 Shekeli 50 za fedha ni sawa na gramu 600. za fedha. Ni lazima amwoe huyo msichana, kwa maana amemfanyia jeuri. Kamwe hawezi kumpa talaka siku zote za maisha yake.
30Mwanaume asimwoe mke wa baba yake; kamwe asidhalilishe kitanda cha baba yake.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 22: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia