Kumbukumbu 21
21
Upatanisho kuhusu mauaji
1Kama mtu akikutwa ameuawa, naye amelala kwenye shamba katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kuimiliki, wala haijulikani ni nani aliyemuua, 2wazee wenu na waamuzi watatoka na kupima umbali kutoka maiti alipolala hadi kwenye miji iliyo jirani. 3Kisha wazee wa ule mji ulio karibu zaidi na yule maiti watamchukua mtamba ambaye hajapata kufanyishwa kazi na ambaye hajafungwa nira, 4na kumpeleka kwenye bonde ambalo halijapata kulimwa au kupandwa mazao na ambapo kuna chemchemi inayotiririka. Huko kwenye hilo bonde, wazee watamvunja yule mtamba shingo. 5Makuhani, hao wana wa Lawi, watasogea mbele, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewachagua kuhudumu na kutoa baraka katika jina la Mwenyezi Mungu, na kuamua mashauri yote ya mabishano na mashambulio. 6Ndipo wazee wote wa mji ulio karibu zaidi na huyo maiti watanawa mikono yao juu ya huyo mtamba ambaye shingo yake imevunjwa huko kwenye bonde, 7nao watatangaza: “Mikono yetu haikumwaga damu hii, wala macho yetu hayakuona likifanyika. 8Ee Mwenyezi Mungu, ukubali upatanisho kwa watu wako Israeli ambao umewakomboa, wala usiwahesabie watu wako hatia ya damu ya mtu asiyekuwa na hatia.” Nayo damu iliyomwagika itakuwa imefanyiwa upatanisho. 9Hivyo mtakuwa mmejitakasa wenyewe kutoka hatia ya kumwaga damu isiyokuwa na hatia, kwa kuwa mmefanya lile lililo sawa mbele za macho ya Mwenyezi Mungu.
Kuoa mwanamke mateka
10Mkienda vitani kupigana na adui zenu, naye Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, akawatia adui mikononi mwenu, nanyi mkachukua mateka, 11kama ukiona miongoni mwa mateka mwanamke mzuri wa sura nawe ukavutiwa naye, unaweza kumtwaa awe mke wako. 12Mlete nyumbani mwako, anyoe nywele na kukata kucha zake, 13avue nguo alizokuwa amevaa alipotekwa. Baada ya kuishi nyumbani mwako na kumwombolezea baba yake na mama yake kwa mwezi mzima, ndipo utakapomwendea, uwe mume wake naye atakuwa mke wako. 14Lakini kama hutaendelea kupendezwa naye, mwache aende popote anapotaka. Kamwe huwezi kumuuza au kumtendea kama mtumwa, kwa sababu utakuwa umemvunjia heshima.
Haki ya mzaliwa wa kwanza
15Kama mwanaume ana wake wawili, naye anampenda mmoja na mwingine hampendi na wote wawili wamemzalia wana wa kiume, lakini mwana mzaliwa wa kwanza ni wa yule mke asiyempenda, 16wakati anapotoa wosia wa mali yake kwa wanawe, kamwe asitoe haki za mzaliwa wa kwanza kwa mwana wa mke ampendaye kwa upendeleo, badala ya mzaliwa hasa wa kwanza, ambaye ni mwana wa mke ambaye hampendi. 17Ni lazima amkubali mwana wa mke asiyempenda kama mzaliwa wa kwanza kwa kumpa sehemu ya vile vyote alivyo navyo maradufu. Mwana huyo ni ishara ya kwanza ya nguvu za baba yake. Haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake yeye.
Mwana mwasi
18Kama mtu ana mwana mkaidi na mwasi ambaye hamtii baba yake na mama yake, na hasikii wazazi wanapomkanya, 19baba yake na mama yake watamleta kwa wazee kwenye lango la mji wake. 20Watawaambia wazee, “Huyu mwanetu ni mkaidi na mwasi. Hatutii sisi, yeye ni mpotovu na mlevi.” 21Kisha wanaume wote wa mjini mwake watampiga kwa mawe hadi afe. Ndivyo imewapasa kuondoa maovu kati yenu. Israeli yote itasikia hili na kuogopa.
Sheria mbalimbali
22Kama mtu ana hatia ya kosa linalompasa kuuawa naye akauawa, mwili wake utaangikwa mtini, 23kamwe msiuache mwili wake mtini usiku kucha. Hakikisheni mnauzika mwili wake siku ile ile, kwa sababu kila mtu anayeangikwa mtini yupo chini ya laana ya Mungu. Msiinajisi nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kama urithi wenu.
Iliyochaguliwa sasa
Kumbukumbu 21: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.