Kumbukumbu 20
20
Kwenda vitani
1Mtakapoenda vitani kupigana na adui zenu na mkaona farasi na magari ya vita na jeshi kubwa kuliko lenu, msiwaogope, kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa kutoka Misri, atakuwa pamoja nanyi. 2Mtakapokaribia kwenda vitani, kuhani atakuja mbele na kuhutubia jeshi. 3Atasema: “Sikia, ee Israeli, leo unaenda vitani kupigana na adui zako. Usife moyo wala usiogope, usitishwe wala usitiwe hofu mbele yao. 4Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ndiye huenda pamoja nanyi kuwapigania dhidi ya adui zenu na kuwapatia ushindi.”
5Maafisa wataliambia jeshi: “Je, kuna yeyote aliyejenga nyumba mpya ambayo haijawekwa wakfu? Yeye na arudi nyumbani, ama sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akaiweka wakfu. 6Je, kuna yeyote aliyepanda shamba la mizabibu na hajaanza kulifurahia? Yeye na arudi nyumbani, au sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akalifurahia. 7Je, kuna yeyote aliyeposa mwanamke na hajamwoa? Yeye na arudi nyumbani, ama sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akamwoa.” 8Kisha maafisa wataongeza haya, “Je, kuna mtu anayeogopa ama kufa moyo? Yeye na arudi nyumbani ili ndugu zake nao wasije wakafa moyo pia.” 9Maafisa watakapomaliza kuzungumza na jeshi, watawateua wakuu wa vikosi.
10Mtakapoenda kushambulia mji, wapeni watu wake masharti ya amani. 11Wakikubali na kuwafungulia malango yao, watu wake wote watakuwa watumwa wa kufanya kazi ngumu, na watawatumikia ninyi. 12Ikiwa watakataa kufanya mapatano ya amani na wakiwaingiza katika vita, basi mtauzingira mji huo. 13Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapouweka mji huo mkononi mwenu, waueni kwa upanga wanaume wote waliomo. 14Kwa upande wa wanawake, watoto, mifugo na kila kitu kingine chochote ndani ya huo mji, mnaweza kuvichukua kama nyara kwa ajili yenu. Nanyi mnaweza kuzitumia hizo nyara ambazo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa kutoka kwa adui zenu. 15Hivi ndivyo mtakavyofanya kwa miji yote iliyo mbali nanyi, ambayo haimilikiwi na mataifa ya karibu.
16Hata hivyo, katika miji ya mataifa ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kama urithi, msiache kitu chochote hai kinachopumua. 17Waangamizeni kabisa Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowaamuru. 18La sivyo, watawafundisha kufuata mambo yote ya machukizo wanayofanya wakiabudu miungu yao, nanyi mtatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
19Mtakapouzunguka mji kwa vita kwa muda mrefu, mkipigana dhidi yake ili kuuteka, msiharibu miti yake kwa kuikata kwa shoka, kwa sababu mtaweza kula matunda yake. Hivyo msiikate. Je, miti hiyo ya mashambani ni watu, hata muizingire? 20Hata hivyo, mnaweza kuikata miti isiyo ya matunda na kuitumia kuuzingira, hadi mji unaofanya vita na ninyi utakapoanguka.
Iliyochaguliwa sasa
Kumbukumbu 20: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.