Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 24

24
Sheria kuhusu ndoa na talaka
1Mtu akimwoa mke na akamchukia kwa sababu ya kuona jambo baya kwake, inawezekana akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani mwake. 2Baada ya mwanamke huyo kuondoka kwake, inawezekana akaolewa na mtu mwingine. 3Mume wake wa pili akichukizwa naye, akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani mwake, au huyo mume wa pili akifa, 4basi yule mume wake wa kwanza, ambaye alimpa talaka, haruhusiwi kumwoa tena baada ya mwanamke huyo kuwa najisi. Hayo yatakuwa machukizo machoni pa Mwenyezi Mungu. Usilete dhambi juu ya nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anakupa kama urithi.
5Kama mtu ameoa karibuni, kamwe asipelekwe vitani au kupewa wajibu mwingine wowote. Kwa mwaka mmoja atakuwa huru kubaki nyumbani ili amfurahishe mke aliyemwoa.
Sheria nyingine
6Usitoe jozi ya mawe ya kusagia, hata ikiwa lile la juu, kuweka rehani kwa ajili ya deni, kwa sababu itakuwa ni kuweka uhai wa mtu kama dhamana.
7Kama mtu akikamatwa akiiba yeyote miongoni mwa ndugu zake wa Waisraeli na kumtenda kama mtumwa au akimuuza, mwizi huyo ni lazima auawe. Nawe utaondoa uovu kutoka miongoni mwenu.
8Pakitokea magonjwa ya ngozi ya kuambukiza, mwe waangalifu sana kufanya sawasawa na maagizo ya makuhani, ambao ni Walawi. Ni lazima mfuate kwa uangalifu yale niliyowaamuru. 9Kumbukeni kile Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alichomfanyia Miriamu njiani baada ya ninyi kutoka Misri.
10Unapomkopesha jirani yako chochote, usiingie nyumbani mwake kutwaa kile anachokitoa kama rehani. 11Ukae nje na umwache huyo mtu uliyemkopesha akuletee hiyo rehani. 12Ikiwa mtu huyo ni maskini, usiende kulala ukiwa na hiyo rehani yake katika milki yako. 13Rudisha vazi lake kabla ya machweo ya jua ili apate kulilalia. Kisha atakushukuru na kitaonekana kama kitendo cha haki mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
14Usimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni nduguyo Mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu. 15Mlipe ujira wake kila siku kabla ya jua kutua, kwa sababu yeye ni maskini na anautegemea ujira huo. La sivyo, anaweza kumlilia Mwenyezi Mungu dhidi yako, nawe ukapata hatia ya dhambi.
16Baba wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.
17Usipotoshe hukumu ya mgeni au yatima, au kuchukua vazi la mjane kama rehani. 18Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa huko Misri, naye Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, akawakomboa kutoka huko. Hii ndiyo sababu ninawaamuru kutenda hili.
19Unapovuna shamba lako na ukasahau mganda, usirudi kuuchukua. Acha kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane, ili Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aweze kukubariki wewe katika kazi zote za mikono yako. 20Unapovuna zeituni kutoka miti yako, usirudie matawi mara ya pili. Acha kilichobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 21Unapochuma zabibu katika shamba lako la mizabibu usirudie tena. Acha zinazobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 22Kumbuka kwamba mlikuwa watumwa katika nchi ya Misri. Ndiyo sababu ninawaamuru kufanya hili.

Iliyochaguliwa sasa

Kumbukumbu 24: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia