Kumbukumbu 25
25
1Watu wanapokuwa na ugomvi, wapeleke mahakamani na waamuzi wataamua shauri hilo; watawaachia wasio na kosa na kuwahukumu wenye hatia. 2Kama mtu mwenye hatia anastahili kupigwa, mwamuzi atamwamuru alale chini ili apigwe mbele yake idadi ya mijeledi kulingana na kosa lake, 3lakini kamwe asipigwe zaidi ya mijeledi arobaini. Akipigwa zaidi ya mijeledi arobaini, nduguyo atadhalilika machoni pako.
4Usimfunge maksai kinywa anapopura nafaka.
5Ikiwa ndugu wanaishi pamoja, naye mmoja wao akafa bila kuacha mwana, kamwe mjane wake asiolewe nje ya jamaa hiyo. Ndugu wa mumewe atamchukua, amwoe na kutimiza wajibu wa shemeji kwake. 6Mwana wa kwanza atakayemzaa atapewa jina la ndugu aliyekufa ili jina lake lisifutike katika Israeli.
7Hata hivyo, ikiwa ndugu huyo wa mume hataki kuoa huyo mke wa nduguye, mjane atawaendea wazee kwenye lango la mji na kusema, “Ndugu wa mume wangu anakataa kuendeleza jina la nduguye katika Israeli. Hataki kutimiza wajibu wa shemeji kwangu.” 8Ndipo wazee wa mji wake watamwita na kuzungumza naye. Kama atashikilia kukataa akisema, “Sitaki kumwoa,” 9mjane wa nduguye atamwendea mbele ya wazee, atamvua kiatu kimoja na kumtemea mate usoni, na kusema, “Hivi ndivyo ambavyo hufanywa kwa mtu ambaye atakataa kuendeleza jamaa ya ndugu yake.” 10Jamaa ya mtu huyo itafahamika katika Israeli kama Jamaa ya Aliyevuliwa Kiatu.
11Ikiwa watu wawili wanapigana na mke wa mmoja wao akaja kumwokoa mumewe na yule anayemshambulia, naye mke huyo akifika na kumkamata sehemu za siri, 12huyo mwanamke utamkata mkono wake. Usimhurumie.
13Usiwe na mawe ya kupimia ya aina mbili katika mkoba wako, moja zito na jingine jepesi. 14Usiwe na vipimo viwili tofauti katika nyumba yako, kimoja kikubwa, kingine kidogo. 15Ni lazima uwe na uzito na vipimo sahihi na vya haki, ili upate kuishi maisha marefu katika nchi anayokupa Mwenyezi Mungu, Mungu wako. 16Kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wako, humchukia yeyote ambaye hufanya mambo kama haya, yeyote anayetenda kwa udanganyifu.
17Kumbuka kile Waamaleki walichowatendea mlipokuwa njiani mkitoka Misri. 18Mlipokuwa mmechoka na kuishiwa nguvu kwa safari yenu, waliwalaki njiani, wakawapiga wale wote waliokuja nyuma. Waamaleki hawakumwogopa Mungu. 19Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapokupa pumziko mbali na adui zako wote wanaokuzunguka katika nchi anayokupa kuimiliki kuwa urithi, utafutilia mbali kumbukumbu lote la Waamaleki chini ya mbingu. Usisahau!
Iliyochaguliwa sasa
Kumbukumbu 25: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.