Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 21:1-9

Kumbukumbu 21:1-9 NENO

Kama mtu akikutwa ameuawa, naye amelala kwenye shamba katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kuimiliki, wala haijulikani ni nani aliyemuua, wazee wenu na waamuzi watatoka na kupima umbali kutoka maiti alipolala hadi kwenye miji iliyo jirani. Kisha wazee wa ule mji ulio karibu zaidi na yule maiti watamchukua mtamba ambaye hajapata kufanyishwa kazi na ambaye hajafungwa nira, na kumpeleka kwenye bonde ambalo halijapata kulimwa au kupandwa mazao na ambapo kuna chemchemi inayotiririka. Huko kwenye hilo bonde, wazee watamvunja yule mtamba shingo. Makuhani, hao wana wa Lawi, watasogea mbele, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewachagua kuhudumu na kutoa baraka katika jina la Mwenyezi Mungu, na kuamua mashauri yote ya mabishano na mashambulio. Ndipo wazee wote wa mji ulio karibu zaidi na huyo maiti watanawa mikono yao juu ya huyo mtamba ambaye shingo yake imevunjwa huko kwenye bonde, nao watatangaza: “Mikono yetu haikumwaga damu hii, wala macho yetu hayakuona likifanyika. Ee Mwenyezi Mungu, ukubali upatanisho kwa watu wako Israeli ambao umewakomboa, wala usiwahesabie watu wako hatia ya damu ya mtu asiyekuwa na hatia.” Nayo damu iliyomwagika itakuwa imefanyiwa upatanisho. Hivyo mtakuwa mmejitakasa wenyewe kutoka hatia ya kumwaga damu isiyokuwa na hatia, kwa kuwa mmefanya lile lililo sawa mbele za macho ya Mwenyezi Mungu.